Kata ya Kalenga,
wilaya ya Iringa, ni mojawapo ya maeneo yanayoakisi hali ngumu ya maisha ya
watoto wengi wa kike na kiume wanaojiingiza katika ajira za utotoni na hiyo
imetokana naugumu wa Maisha ya walezi wao.
Watoto hao ambao wengi
wao wanalelewa na bibi zao kutokana na wazazi wao kukimbilia miji mikubwa ili
kupata Maisha bora, wamejikuta wakiingia kwenye harakati za kila siku za
kutafuta chupa za maji za plastiki na vyuma chakavu ili waweze kuuza na
kujipatia kipato kitakacho wasaidia wao na walezi wao.
Hata hivyo, hali hiyo hiyo inasababisha, watoto kushindwa kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu wanayostahili, pamoja na
kuwaweka katika mazingira hatarishi kiafya na kimwili.
Ajira za utotoni ni
aina ya kazi ambazo mtoto haistahili kufanya kwa umri wake, Kazi hizi, kama
vile kubeba matofali, kuuza chupa za plastiki na vyuma chakavu, humzuia mtoto
kupata elimu na inaweza kuathiri afya, usalama, tabia, na makuzi yake.
Hata hivyo, watoto hao
wamesema wakiwa katika harakati za
kutafuta vitu hivyo mekuwa wanakutana na
changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, ukatali na mazingira
hatarishi.
Kwa upande wao, Wakazi
wa Kata ya Kalenga wamesema kuwa sababu kuu, inayochangia watoto kujiingiza
katika ajira za aina hiyo ni hali duni za familia.
Wamesema wazazi wengi
wanashindwa kutoa huduma bora kwa watoto wao kutokana na hali duni ya kiuchumi,
na wamnaume wengine wanakimbia majukumu yao ya familia na kuwaacha wake na
watoto wao bila msaada wowote, huku baadhi ya watoto wakiachwa na bibi zao
wakati wazazi wao wanapokimbilia miji mikubwa kutafuta maisha bora.
Martin Chuwa, Afisa
Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa Maafisa Jamii Tanzania Bara,
amesema kuwa wilaya ya Iringa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto
waliotelekezwa na wazazi wao, na kwa sasa, wilaya hiyo ina jumla ya watoto
8,600 waliotelekezwa.
Chuwa amesema athari
za ajira za utotoni si tu kwa maendeleo ya watoto, bali pia zinaongeza hatari
ya watoto kukutana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia. Watoto wanajikuta
wakiwa katika mazingira hatarishi, ambapo wanadhulumiwa na kukosa haki zao za
msingi, kama vile elimu na usalama wa kisheria.
Mwanasheria wa
kijitegemea, Baraka Kimata, amesisitiza umuhimu wa watoto katika jamii na
kuzungumzia haki za watoto ambazo zimetambuliwa na sheria za kitaifa na
mikataba ya kimataifa.
Kimata amesema kuwa
watoto wanastahili kupata haki za msingi kama vile elimu, afya, usalama, na
ulinzi wa kisheria, na kuongeza kuwa watoto wanapaswa kukua katika mazingira
salama na yenye maendeleo, na ni kosa kwa mzazi au mlezi kumnyima mtoto wake
haki hizo za kisheria.
Katika kukabiliana na
changamoto hiyo, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeanzisha juhudi za
kupambana na ukatili wa kijinsia, na sasa umejikita katika wilaya ya Iringa,
hasa Kata ya Kalenga.
TGNP imefanikiwa kutoa
mafunzo ya siku tano kwa wakazi wa kata hiyo, ambapo mafunzo haya yamelenga
kuelimisha jamii kuhusu njia za kupambana na ukatili wa kijinsia na umuhimu wa
kuwashirikisha wanaume katika masuala ya usawa wa kijinsia.
Rose Mwaisiko,
Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Kalenga, amesema, kuwa
mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa wa wazazi na walezi kuhusu athari za
ajira kwa Watoto, Pamoja na kupunguza
changamoto.
Changamoto za ajira
kwa watoto katika Kata ya Kalenga ni kielelezo cha hali ngumu inayokumba jamii
nyingi nchini Tanzania, Watoto wengi wanajikuta wakifanya kazi ambazo siyo tu
zinawazuia kupata elimu, bali pia zinawaweka katika hatari ya kutelekezwa na
kukosa haki zao za msingi.
Hata hivyo, juhudi za
mashirika kama TGNP na uhamasishaji wa jamii unaweza kusaidia kutatua
changamoto hizi na kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa za kukua katika
mazingira salama, bora, na yenye maendeleo.
Kwa pamoja, jamii,
wazazi, na taasisi za serikali wanahitajika kuunga mkono juhudi hizi ili
kuhakikisha watoto wanakuwa na maisha bora, mbali na kazi za kulazimishwa.
0 Comments