Yalalamikia Kutumikishwa kwa Wanufaika wa TASAF na Ahadi ya Kulipa Sh. 30,000 Kila Mzee
Na Ashrack Miraji
CHAMA cha The Nation League for Democracy (NLD) kimezindua rasmi kampeni zake kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu. Katika uzinduzi huo, chama hicho kimejitolea kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi, huku kikilaani vikali vitendo vya Serikali kuwatumikisha wanufaika wa TASAF kwa kazi ngumu kama vile kuchimba mitaro, visima na mabwawa.
Uzinduzi wa kampeni ulifanyika katika kijiji cha Kwedikwazu wilayani Handeni, ambapo NLD kimesimamisha wagombea katika vijiji na mitaa mbalimbali ndani ya wilaya hiyo. Akizungumza na wakazi wa Handeni, Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, alisema chama hicho kimejitokeza kwa nguvu na kimetangaza kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi, hasa katika kuongeza ajira na kuboresha huduma za kijamii.
"Tunatarajia Ushindi Katika Kila Kijiji na Mtaa Tunaposimamisha Wagombea"
Doyo alieleza kuwa NLD kimesimamisha wagombea katika zaidi ya vijiji 700 nchini, na kwamba kimejipanga kuhakikisha kinashinda katika maeneo yote. "Tumesimamisha wagombea kwenye mitaa na vijiji vingi nchini, na katika Kijiji hiki cha Kwedikwazu, tumesimamisha wagombea kwa kila mtaa na kijiji. Tuna wagombea wanaokubalika na wana sifa nzuri, hivyo hatuoni sababu ya kutoshinda," alisema Doyo.
Aliongeza kuwa wilaya ya Handeni, ingawa ina rasilimali za madini, bado haijafaidi kutokana na utawala wa sasa. "Kijiji hiki kina madini, lakini katika akaunti ya kijiji hakuna hata shilingi mia mbovu. Hii inaonyesha kwamba uongozi wa sasa umeshindwa kusimamia maslahi ya wananchi. NLD ikishika madaraka, tutahakikisha madini ya kijiji hiki yanatumika kwa manufaa ya wakazi, tutawekeza katika ofisi bora na madarasa ya kisasa kwa watoto," alisema Doyo.
"TASAF: Wanufaika Wanatumikishwa Kazi ngumu Badala ya Kukidhi Mahitaji Yao"
Doyo pia alizungumzia changamoto zinazowakumba wanufaika wa TASAF, akisema kuwa serikali imekuwa ikiwalazimisha kufanya kazi ngumu badala ya kuwasaidia kwa malengo ya programu hiyo. "Serikali imekuwa ikiwatumikisha wazee na vijana wa TASAF kufanya kazi ngumu, kama vile kuchimba visima, mitaro, na mabwawa. Hii ni kinyume na malengo ya TASAF, ambayo inapaswa kusaidia kaya maskini, hasa wazee," alisema Doyo.
Aliahidi kuwa NLD itahakikisha kila mzee anayepokea msaada wa TASAF atapokea Sh. 30,000 kila mwezi kama msaada bila kulazimika kufanya kazi ngumu. "Niko tayari kulipia kila mzee Sh. 30,000 kila mwezi, bila kufanya kazi ngumu. Huu utakuwa ni ahadi yetu kwa wazee wa Kijiji hiki endapo tutashinda uchaguzi," alisisitiza Doyo.
0 Comments