Na Shemsa Mussa -Matukio daima Media
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa, amewataka wakazi wa Mkoa huo kuendelea kuwa watulivu na kuzingatia taratibu za uchaguzi.
Akizungumza baada ya kupiga kura kwenye kituo cha uwanja wa ndege katika mtaa wa Pwani kata Miembeni Novemba 27, 2024
Mwassa amewasihi Wananchi warudi nyumbani na kupumzika huku wakisubili matokeo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na usalama huku akionya dhidi ya vurugu ambazo hazikubaliki katika utamaduni na mila za mkoa huo.
"Mkoa wa Kagera unajulikana kwa ustarabu, utulivu, busara na hekima Hatuwezi kukubali uchaguzi wetu uleta mtafaruku," alisema kiongozi huyo.
Wakati wa ziara hiyo, Mwassa ameambatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Jacobo Nkwera, na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima, ambapo Viongozi hao walitembelea vituo kadhaa vya kupigia kura kama vile Kilima Hewa, Katatwolansi, Kashai Halisi, Miembeni, na Kahororo, wakitathmini mwenendo wa uchaguzi.
Mwassa amewahakikishia wananchi usalama na amani, akiwataka kuzingatia usalama wao na wa wengine.
"Nimefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika vituo vyote, na inaonyesha kuwa huenda tukamaliza mapema katika Manispaa ya Bukoba"alisema Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Kagera unategemea kuwa na wapiga kura zaidi ya Milioni 1.5 na vituo vya kupigia kura 4,012.
0 Comments