Header Ads Widget

AGRREY MWANRI :BALOZI WA PAMBA ALIYEJIKITA KUFUFUA DHAHABU NYEUPE

Balozi wa Pamba nchini Agrey Mwanri akiwaonyesha wakulima wa Pamba wa kijiji cha Imalanguzu wilaya ya Igunga mkoani Tabora juu ya matumizi sahihi ya nozeli kwenye pambu ya matabi wakati wa upuliziaji wadudu shambani.

Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, Renatus Philibert (wa tatu kushoto) akikagua shamba la mkulima wa kijiji cha Nkoma wilayani Meatu, akiwa ameambatana na Maafisa ugani wa mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT). (Picha zote na COSTANTINE MATHIAS)

BALOZI wa Pamba nchini Agrey Mwanri (katikati) akiwaonyesha wakulima  wa kijiji cha Imalanguzu wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora namna bora ya kupulizia sumu za kuuwa wadudu wanaoshambulia zao la Pamba.

Na Matukio Daima App.

AGRREY Mwanri (69), siyo jina geni sana kwenye Siasa na Masikio ya Watanzania, kwani amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Amekuwa maarufu kupitia msemo wake “Injinia…Soma hiyo”, lakini hivi karibuni aligeukia Uinjilisti katika Kanisa la KKKT baada ya kustaafu utumishi wa Umma.

Bodi ya Pamba nchini (TCB) ilimpa jukumu la kuwa Balozi wa Pamba kwa kuzungukia Mikoa, wilaya na vijiji vinavyolima pamba ili kuelimisha wakulima juu ya kanuni za kilimo bora cha pamba, kuongeza tija na kurejesha zao hilo maarufu kama Dhahabu Nyeupe lililokuwa likisuasua uzalishaji.

Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa Pamba ni moja kati ya Mazao matano ya Kimkakati na kibiashara ambayo serikali ya awamu ya sita imejikita kuyasimamia ili kuhakikisha yanazalishwa kwa tija na kuongeza pato la taifa pia kukuza uchumi wa mkulima.

Zao hili linalimwa katika mikoa 17 nchini ambayo ni Simiyu, Geita, Shinyanga, Mara, Kigoma, Katavi, Mwanza, Morogoro, Tabora, Kagera, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Pwani, Iringa, Tanga na Singida.

Kwa Mujibu wa Bodi ya Pamba, zao hilo huingiza zaidi fedha za kigeni ambapo katika msimu wa 2022/2023, pamba ililiingizia taifa takribani dola za marekani milioni 227.1.

Takwimu za TCB zinabainisha kuwa, takribani wakulima 600,000 wanajihusisha na kilimo cha pamba nchini na Mkoa wa Simiyu unatajwa kuwa kinara kwa uzalishaji.

Hivyo Mwanri amekuwa akizungukia wakulima wa pamba na kutoa elimu tangu kuaanda mashamba, kulima, kupanda, kupunguzia miche, kupulizia wadudu hadi uvunaji ili kulinda ubora wa zao hilo.

 

Anawataka wakulima kuzingatia maelekezo ya Wataalamu wa Kilimo ikiwemo kusimamia upuliziaji wa dawa ili waweze kudhibiti wadudu wanaoshambulia pamba na kusababisha kupata mavuno haba.

Anawaelekeza kukagua mashamba yao mara kwa mara na kuwashirikisha maafisa kilimo ili wawaelekeze namna sahihi ya kudhibiti wadudu kama chawa jani na funza wanaofyonza na kuharibu vitumba.

Anaongeza kuwa lengo la serikali ni kuzalisha Tani Mil. Moja ifikapo 2025 ambapo Tanzania itaweza kuongeza uzalishaji wa pamba katika bara la Afrika na kwamba wananchi watajiinua kiuchumi.

‘’Tunapoteza pamba nyingi kwa sababu tumeshindwa kudhibiti wadudu waharibifu wa zao la pamba ikiwemo chawa jani na kidung’ata…tunatoa elimu hii kwa mkulima kutokana na kutodhibiti masalia, kanuni ya pamba inamtaka mkulima ang’oe masala yote ili kudhibiti wadudu’’ anasema Mwanri.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga anawataka wanasiasa kuacha kupinga sayansi kutoka kwa wataalamu wa pamba ili kulinda ubora wa zao hilo.

Anawataka wataalamu wa kilimo kuendelea kuelimisha wakulima wa pamba kupitisha mashamba darasa katika maeneo yao ili kuongeza tija.

Mkaguzi wa Pamba kutoka wilaya ya Igunga, Venance Kankutebe anasema elimu inayotolewa na Balozi wa Pamba (Mwanri), itawasaidia wakulima kuongeza tija ya uzalishaji.

Anasema tangu wameanza kampeni ya kuelimisha jamii juu ya namna bora na matumizi sahihi ya viua wadudu mavuno yameongezeka na mwitikio wa upuliziaji kwa wakulima na matumizi ya nozeli sahihi yamezingatiwa.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo wilaya ya Meatu, Thomas Shilabu amesema wilaya hiyo inatarajia kuvuna tani 42,000 katika msimu wa 2023/24 na kwamba wameshapokea chupa (ekapaki) 555,400 na maboza (bomm spray) ili kuleta ufanisi katika kilimo cha pamba.

‘’Tunashukuru Serikali ya Dkt. Samia kwa kutuwezesha bajeti ya kujenga nyumba za maafisa ugani vijijini ili waweze kuishi huko na kuhudumia wakulima, tumepata vifaa vya kupimia udongo kwenye mashamba ya wakulima ili wajue hali ya udongo wao ili kuinua kilimo na kufikia tija’’ anasema Shilabu.

Shilabu anaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuajiri Maafisa Ugani kupita Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT) ambao wameongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wakulima wa pamba na mazao mengine.

Anaeleza kuwa wataalamu hao wameshasambazwa vijijini ili kuwasaidia wakulima kulima kisasa na kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba na kwamba serikali imeanza kupata takwimu halisi na sahihi za wakulima na mashamba yao.

Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilaya ya Meatu, Renatus Philibert anasema serikali imeendelea kutatua suala la upatikanaji wa  pembejeo na mifumo ya masoko ambapo awali ukosefu wa maafisa ugani ulikuwa ukiwakwamisha wakulima kuzalisha wa pamba kwa tija.

Anasema kupitia Mpango wa BBT, serikali imeleta Maafisa Ugani 47 katika wilaya hiyo ambao wamesambazwa vijijini kwa ajili ya kusaidiana na Maafisa ugani wa serikali waweze kumwelimisha na kumfikia mkulima.

‘’Wamesambaa kwenye vijiji katika wilaya hii, wamesaidia kuhakiki mashamba na kumhudumia mkulima kulingana na mahitaji yake…wakulima wameanza kunufaika kwa kupata elimu ya vitendo moja kwa moja mashambani’’ anasema Renatus.

Afisa Kilimo kupitia BBT, kijiji cha Nkoma Mainazam Kiduka anasema awali kijiji hicho kulitambuliwa kuwa na ekari 4000 za pamba ambazo siyo halisi, lakini baada ya ujio wao wamebaini kuwa wakulima wengi walikuwa wanadanganya taarifa ili kupata pembejeo kwa wingi.

‘’Tumegundua kwamba, wakulima wengi walikuwa wanadanganya ili kupata mbegu au pembejeo, uhalisia mkulima ana ekari nne lakini anataja ekari 20 ili apate dawa nyingi…ujio wetu tumebaini hilo na sasa dawa zimeanza kuwatosha wakulima’’ anasema.

Msigwa Marco kutoka BBT, kijiji cha Itaba anaipongeza serikali kwa kuongeza maafisa ugani ili waongeze tija katika kilimo cha pamba ambapo hapo awali wakulima wengi walikuwa hawajafikiwa na huduma hiyo hali iliyosababisha kushindwa kutambua wadudu na madhara yake.

Wakulima wa Pamba wameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha huduma za Ugani pamoja na kuongeza maafisa kilimo kupitia Mpango wa jenga Kesho Bora ambao wameanza kuleta mapinduzi katika sekta ya Kilimo.

Shija Homela Mkazi wa Imalanguzu naipongeza serikali kwa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu huku akisisitiza kuendelea kutoa dawa mapema ili wakulima waweze kudhibiti wadudu wanaoshambulia pamba kwa wakati. 

Anasema baada ya serikali kuimairisha huduma hizo, wakulima hao wanatarajia kuongeza uzalishaji wa pamba, kukuza pato la taifa na kuimarisha uchumi wa mkulima mmoja mmoja.

Mahizi Jilala, mkulima wa kijiji cha Nkoma anasema anaipongeza serikali kwa kuwajali wakulima juu ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, kuajiri watalamu wa kilimo kila kijiji ambao wameanza kuwafikia wakulima moja kwa moja na kuwafundisha kwa vitendo.

Jilala anawataka wakulima wa pamba kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili waweze kuleta tija ya kupata mavuno mengi huku akiiomba serikali kuongeza maafisa kilimo ili watoe elimu ya kilimo bora kabla ya kuanza kulima.

Shole Phares, mkazi wa Busule Nkoma anaipongeza serikali kupitia Bodi ya Pamba kwa kuajiri maafisa kilimo ambao wamemwezesha kulima kisasa huku akitarajia kupata mavuno mengi kutokana na kuzingatia maelekezo ya watalaam.

Anasema, katika msimu huu wa 2023/24 anategemea kuvuna kilo 1200 kwa ekari moja kutoka kilo 800 kwa ekari alizovuna mwaka jana, baada ya kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba ikiwemo upandaji wa mistari na kwa wakati.

MWISHO.

 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI