Header Ads Widget

VIONGOZI WA DINI WATOA NENO UZINDUZI DAFTARI LA WAPIGA KURA



Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

 ZOEZI la uandikishaji wa wakaazi wa mkoa Kigoma kwenye daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa umeanza mkoani Kigoma huku viongozi wa dini na serikali wakitaka watu kujitokeza kuandikishwa  lakini pia kufichua wageni wanaotaka kujipenyeza kuandikishwa.

 


Shekhe wa mkoa Kigoma, Hassan Iddi Kiburwa akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kujiandikisha katika kituo cha Mtaa wa Bugogwa alisema kuwa kujiandikisha kwenye daftari hilo la mkaazi ndiyo njia pekee itakayowapa wananchi haki ya kupiga kura Novemba 27 mwaka huu bila kuwa na kizuizi chochote.

 

Kwa upande wake Padri George Mhanuka, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kigoma akizungumza baada ya kujiandikisha katika kituo cha Shule ya Msingi Kigoma akiwasilisha ujumbe wa Askofu wa jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola  alisema kuwa kujiandikisha katika daftari hilo kwa ajili ya zoezi la kupiga kura inatoa haki ya msingi ya kiraia katika kuchagua viongozi wanaowataka bila kushurutishwa, hivyo ametoa wito watu wote kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.



 Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Shaban Chuachua aliyejiandikisha katika kituo cha ofisi ya mtendaji wa kata ya Kigoma alisema kuwa udhibiti umewekwa ili kuzuia wageni kujiandikisha kwenye daftari hilo.



Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari baada ya kujiandikisha na kuzindua rasmi zoezi hilo Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Hassan Rugwa alisema kuwa hadi sasa watu milioni 1.3 wenye  sifa ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo wanatarajia kuandikishwa kukiwa na vituo 2252 ambavyo vimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo katika halmashauri zote nane za mkoa Kigoma.



Kufuatia kuanza kwa zoezi hilo Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wenye sifa kujitokeza kujiandikisha huku akitaka uwepo usimamizi thabiti kuzuia wageni kutoka nje kujiandikisha kwenye daftari hilo.

 

 

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI