Header Ads Widget

MAKALA:CHANGAMOTO ZA WANAWAKE KATIKA KUPATA NAFASI ZA UONGOZI ZANZIBAR

 


Dkt. Mzuri Issa - Mkurugenzi wa TANWA - ZNZ

NA THABIT HAMIDU, MATUKIO DAIMA MEDIA ZANZIBAR 

Bahati Issa Suleiman, mwenye umri wa miaka 51 na mkazi wa Kikungwi, Mkoa wa Kusini Unguja, ni mfano halisi wa changamoto wanazokutana nazo wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi.

 Bahati, ambaye aliwania nafasi ya udiwani wa wadi ya Bungi katika uchaguzi wa 2020 kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), pia ni mwanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

 Katika simulizi yake, Bahati anaeleza changamoto alizopitia na sababu zilizomkwamisha kufanikisha ndoto yake ya kuwa kiongozi.

Bahati alianza safari ya kisiasa mwaka 2015 baada ya kupatiwa mafunzo na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA-Zanzibar). Alijaribu nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM, lakini mara zote hakuweza kufanikiwa.

“Licha ya kushindwa mara kadhaa, sikuweza kukata tamaa. Nilijikuta nikikabiliana na mitazamo potofu kutoka kwa watu waliokuwa wakidharau uwezo wa mwanamke kuwa kiongozi,” anasema Bahati.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa inayowakwamisha wanawake wengi ni ukosefu wa kujiamini.

“Wanawake wengi wanashindwa kujitokeza kugombea, na hata wanapojitokeza, hawaungwi mkono na wenzao. 

Tunaogopa kuthibitisha kwamba mwanamke anaweza kuwa kiongozi bora,” anaeleza.

 Pamoja na changamoto hizo, Bahati anasisitiza kuwa anaendelea kuwa na matumaini na bado ana ndoto ya kushika nafasi ya uongozi siku za usoni.


Wakati Zanzibar ikiendelea kusukuma ajenda ya usawa wa kijinsia (50 kwa 50) katika nafasi za uongozi, nchi kama Rwanda imefanikiwa kupiga hatua, ambapo asilimia 60 ya viongozi ni wanawake. 


Hali hii inaonesha kwamba dhana ya kuwa wanawake hawawezi kuongoza si ya kweli.

Kwa Tanzania, jumla ya wapiga kura 29.1 milioni walishiriki uchaguzi wa mwaka 2020, huku Zanzibar ikiwa na wapiga kura 566,352.

 Mwaka huo kulikuwa na mwamko mkubwa wa wanawake kugombea, na wanawake wapatao 300 walijitokeza kupitia vyama mbalimbali.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Almas Mohammed, anaeleza kuwa vikwazo vinavyowakabili wanawake ni pamoja na mitazamo hasi, majukumu ya kifamilia, ubaguzi wa kijinsia, na mfumo dume unaotawala siasa na serikali. 

Pia, ukosefu wa uungwaji mkono kutoka ndani ya vyama na jamii ni changamoto kubwa.

“Jamii inapaswa kuondokana na dhana potofu kwamba mwanamke hawezi kuongoza, kwani wanawake wengi duniani wanafanya mambo makubwa kuliko wanaume,” anasema Almas.

Ripoti ya TAMWA-Zanzibar inaonesha kuwa katika uchaguzi wa 2020, wanawake waliopata nafasi ya uwakilishi katika majimbo ya Zanzibar walikuwa nane tu kati ya 50. 

Wabunge wanawake waliowakilisha Zanzibar walikuwa wanne, mawaziri sita (asilimia 33), makatibu wakuu saba (asilimia 39), huku mkuu wa mkoa mmoja tu akiwa mwanamke.

 Wakuu wa wilaya walikuwa wanne, wakifikia asilimia 36, na masheha wanawake walikuwa 68 kati ya 389, sawa na asilimia 17.

Ukosefu wa Rasilimali na Umuhimu wa Kuwawezesha Wanawake katika hili Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA-Zanzibar, anasema ukosefu wa rasilimali fedha ni mojawapo ya changamoto kubwa inayowakwamisha wanawake kufikia malengo ya kuwa viongozi.

“Ni muhimu kuwawezesha wanawake kiuchumi ili waweze kushindana kwenye medani za siasa na kufanikisha ajenda ya usawa wa kijinsia ya 50 kwa 50,” anasema Dkt. Mzuri.

Tunu Juma Kondo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), anaeleza kuwa baadhi ya wanawake hawatambui haki yao ya kugombea nafasi za uongozi.

“Kwa muda mrefu, watu walidhani kuwa uongozi ni kwa watu maalum pekee, hali iliyopelekea wanawake wengi kusita kujitokeza,” anasema Tunu.

Ushirikiano wa Vyama vya Siasa na Tume ya Uchaguzi

Sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 inahimiza usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa sera za vyama. 

Hata hivyo, utafiti wa mwaka 2013 uliobaini kuwa vyama vingi bado havijaweka mazingira mazuri kwa wagombea wanawake, unathibitisha kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unakumbwa na changamoto.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, anakiri kuwepo kwa changamoto za kijinsia lakini anasisitiza kuwa ZEC inatekeleza sera jumuishi inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jinsia zote katika siasa.


Bahati Issa Suleiman ni mfano wa wanawake wengi wanaojitahidi kupambana na changamoto mbalimbali ili kufanikisha ndoto zao za uongozi. 

Pamoja na vikwazo vya kijamii na kisiasa, wanawake wanapaswa kuendelea kujiamini na kushirikiana kuleta mabadiliko.

 Uhamasishaji na kuwawezesha wanawake kiuchumi ni hatua muhimu katika kufanikisha ajenda ya usawa wa kijinsia.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI