Na Francis Godwin
UJIO wa tuzo ya Samia Kalamu Awards ni dhahabu ya kamera na Kalamu ya Mwandishi wa habari Tanzania .
Ni ukweli usiopingika kuwa waandishi wa habari Nchini Tanzania wamekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya Taifa hili na mchango wao umeendelea kuthaminishwa na baadhi ya Taasisi za kiraia na hata zile za serikali .
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),kilichoanza mwaka 1987 likiwa na idadi ya wanachama 13 pamoja na kazi kubwa ya kupigania usawa wa kijinsia hasa wa wanawake na wasichana nchini TAMWA ambacho kwa sasa kimepiga hatua na kuwa na wanachama zaidi 250 kimekuwa Cha Cha mfano kwa kuja na mpango wa kuthaminisha Kalamu ya Mwandishi kupitia tuzo ya heshima ijulikanayo kama SAMIA KALAMU AWARDS.
Jina Pekee la tuzo hii ni heshima kwa mshindi na sawa na Kalamu dhahabu kwa mwandishi wa habari iliyokuwa ikisuburiwa kwa muda mrefu .
TAMWA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamezindua rasmi Samia Kalamu Awards kwa lengo la kuimarisha ubora wa uandishi wa habari na kuhamasisha wanahabari kuandika kwa uzalendo, uwajibikaji, na kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma.
Tuzo hizi, ambazo zimepangwa kutolewa kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 20, 2024, ni sehemu ya juhudi za kuinua uandishi wa ndani na kutoa msukumo wa maendeleo kupitia maudhui yanayolenga mahitaji ya Watanzania.
Lengo la Tuzo na Umuhimu kwa Tasnia ya Habari za Samia Kalamu Awards zinalenga kuhamasisha wanahabari kuandika na kuchapisha makala zenye maudhui ya kina, hasa kuhusu maendeleo ya kijamii, uzalendo, na uwajibikaji.
Ni ukweli kuwa Katika mazingira ya sasa ya utandawazi, vyombo vya habari vimekuwa vikikumbwa na changamoto ya kutojikita ipasavyo katika masuala ya ndani, huku yakitoa kipaumbele kwa burudani na maudhui ya nje.
Dkt. Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA, alibainisha kuwa tuzo hizi zinalenga kurejesha taswira chanya ya uandishi wa habari nchini kwa kuhamasisha makala bora zinazochochea mabadiliko ya kijamii.
"Tunataka kuona waandishi wakijituma kuandika makala za kina zinazochunguza changamoto na fursa zilizopo nchini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa," alisema Dkt. Reuben wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo katika Serena Hotel, Dar es Salaam.
Kwa kuanzisha tuzo hizi, TAMWA na TCRA wanataka kupanua wigo wa fursa kwa wanahabari ili kuhakikisha kazi zao zinathaminiwa na zinachangia katika maendeleo ya jamii.
Tuzo hizi zinakwenda sambamba na kuwahimiza waandishi kutumia uandishi wao kuimarisha uzalendo na uwajibikaji miongoni mwa wananchi.
Katika tuzo hizi makundi ya tuzo na Vigezo vya Ushiriki katika tuzo za Samia Kalamu Awards zimegawanywa katika makundi matatu makuu:
Kuwa na tuzo Maalumu za Kitaifa Kwa makala zinazoshughulikia masuala ya msingi ya kitaifa kama vile maendeleo ya kijamii, siasa, na uchumi.
Pili tuzo za Vyombo vya Habari Kwa vyombo vya habari vinavyoonyesha jitihada za kukuza maadili na uwajibikaji kupitia maudhui bora.
Tatu ni tuzo za Kisekta Kwa makala zinazojikita katika sekta muhimu kama afya, elimu, kilimo, nishati, na miundombinu.
Anasema ili kushiriki, kazi zinazowasilishwa lazima ziwe zimetangazwa au kuchapishwa kati ya Januari 1 na Oktoba 26, 2024.
Aidha, makala hizo zinaweza kuwa katika Kiswahili au Kiingereza na zinatakiwa kuwa na utafiti wa kina, zikijumuisha vyanzo angalau vinne vya taarifa.
Kazi zote zinapaswa kuwa za kipekee na zisizowahi kushindanishwa katika mashindano mengine.
Huku mchakato wa Kupiga Kura na Uchaguzi wa Washindi wa Samia Kalamu Awards zitatoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa kupiga kura, ambapo kura za wananchi zitachangia asilimia 60 ya matokeo ya mwisho.
Majaji walioteuliwa watachangia asilimia 40 ya maamuzi hayo Kupiga kura kutawezekana kupitia mfumo wa SMS kwa kutumia namba fupi 15200 na pia kupitia tovuti rasmi ya tuzo (https://samiaawards.tz).
Mchakato huu wa uwazi unalenga kuhakikisha kuwa washindi wanapatikana kwa haki na kazi bora zinatambuliwa na kuthaminiwa.
Washindi wa tuzo hizo watajishindia zawadi za fedha na fursa za kushiriki mafunzo ya kitaalamu zaidi ili kuboresha uandishi wao.
Tambua kuwa ili Kila jambo linanfike kwa ufanisi lazima maelekezo ama Mafunzo ya nini Cha kuzingatia yatolewe hivyo mafunzo kwa Wanahabari zaidi ya 250 nchini yalitoleea hii ilikuwa ni hatua Muhimu Kuelekea Uandishi Bora kabla ya uzinduzi wa tuzo hizi, TAMWA na TCRA waliendesha mafunzo kwa wanahabari zaidi ya 2,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Mafunzo haya yalijikita katika kuimarisha weledi na maadili ya uandishi wa habari.
"Lengo letu lilikuwa kuwafikia wanahabari 1,000, lakini tumefanikiwa kutoa mafunzo kwa zaidi ya waandishi 2,000, jambo ambalo linaonyesha mwitikio chanya kutoka kwa wanahabari," alisema
Anasema kuwa tuzo hizi zimepewa jina la Samia Kalamu Awards kwa heshima ya Rais Samia Suluhu Hassan, rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania, kwa mchango wake katika kuimarisha maendeleo na maadili ya kitaifa.
Anasema kwa kuanzisha tuzo hizi, TAMWA na TCRA wanatarajia kujenga urithi endelevu wa uandishi wa habari unaochochea maendeleo na kuchangia katika kuimarisha uzalendo nchini.
"Tuzo hizi zitakuwa endelevu na zitatolewa kila mwaka ili kuhakikisha kuwa wanahabari wanaendelea kuandika makala bora zinazolenga kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.
Anasema tuzo za Samia Kalamu Awards zinawakilisha fursa adimu kwa waandishi wa habari nchini Tanzania kujitokeza na kushindana kwa weledi.
Kuwa tuzo hizi si tu zawadi za fedha, bali pia ni jukwaa la kutambua juhudi za wanahabari wanaojitahidi kuleta mabadiliko kupitia uandishi wao.
Kwa kuwasilisha kazi zao kupitia mifumo rasmi iliyotajwa, wanahabari wanahimizwa kuchangamkia fursa hii ili kuonyesha umahiri wao katika uandishi wa ndani.
Anasema kuwa hii pia itasaidia kuimarisha tasnia ya habari kwa ujumla na kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kitaifa.
Mhandisi Andrew Kisaka, Meneja wa Huduma za Utangazaji TCRA anasema kuwa Mafunzo hayo yalijumuisha waandishi wa habari, watangazaji, wahariri, na watengenezaji maudhui, lengo likiwa ni kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika tuzo hizi.
Mafanikio ya mafunzo haya tayari yameanza kuonekana, huku wanahabari waliopitia mafunzo hayo wakieleza matumaini yao kwa mustakabali wa tasnia ya habari nchini.
Samira Yusuph na Matias Canal, baadhi ya wanahabari waliopata mafunzo hayo, waliipongeza TAMWA na TCRA kwa jitihada hizo.
"Tuzo hizi si tu kwamba zitatambua kazi bora za wanahabari, bali pia zitawapa motisha ya kufanya utafiti wa kina na kuchapisha makala zenye tija kwa taifa," alisema Samira.
Christopher Salimgwa na Ashura John ni wakazi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam ambao ni wafuatiliaji Wazuri wa vyombo vya habari za Utangazaji na vile vya mitandaoni wanasema kuwa wanapongeza ujio wa tuzo hizo utachochea ari ya waandishi kuandika habari zenye mvuto badala ya kuendelea kuandika habari za udaku na zile zinazozua taharuki kwa jamii.
Salingwa anasema ni vema waandishi kushiriki kwa wingi tuzo hizo na wasitazame kushinda bali wazingatie heshima ya kazi yao Jinsi ilivyoheshimishwa.
Huku Ashura akitaka TAMWA na TCRA kuwajengea Uwezo zaidi waandishi ili kupunguza maudhui yasiyofaa kwa jamii.
Anasema tuzo hizo ni Heshima kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa wadau mbali mbali Wanapaswa kuunga mkono kwa kudhamini tuzo hizo ili Kuhamasisha zaidi waandishi na vyombo vya habari Nchini kuandika kizalendo zaidi .
Ni ukweli keamba tuzo hizi zinatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha kuimarisha maadili na uzalendo, huku zikitoa msukumo kwa wanahabari kufanya utafiti wa kina na kuchapisha makala zenye tija kwa taifa.
Hivyo waandishi watakaojitokeza kushiriki tuzo hizi si fursa ya pesa na tuzo Pekee ndio watapata bali watakuwa wamechangia kwa Kalamu zao katika maendeleo ya taifa kwa ujumla ndio maana unaweza Jinsi gani Kalamu na kamera ya Mwandishi inapogeuka kuwa dhahabu kwake .
MWANDISHI WA MAKALA HII FRANCIS GODWIN NI MTAYARISHAJI MAUDHUI KATIKA MTANDAO WA MATUKIO DAIMA MEDIA PIA NI MWANDISHI WA MAGAZETI MBALI MBALI ANAPATIKANA KWA NAMBA 0754026299 BARUA PEPE: matukiodaima3@gmail.com
0 Comments