NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameagiza Bodi ya maji bonde la Pangani, Tume ya Taifa ya umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Same kuhakikisha ndani ya siku saba (7) mgogoro wa matumizi ya maji kwenye mfereji wa umwagiliaji Shakaka unao hudumia maeneo matano ya Kata ya Vuje na Maore ikiwemo wakazi wa Kitongoji cha Kalung'oyo (Vuje) uwe umepatiwa ufumbuzi.
Ametoa agizo hilo akiwa Kitongoji cha Kalung'oyo kwenye mkutano wa hadhara wa kutatua kero na malalamiko mbalimbali ya wakazi wa eneo hilo, akisisitiza kuitishwa kwa mkutano wa hadhara maalum kwaajili ya wananchi kufanya Uchaguzi kupatikane viongozi watakao simamia shughuli kwenye mfereji huo.
“Watu wa bonde msiondoke huku mkajipange vizuri na watu wa Halmashauri na Tume ya Taifa ya umwagiliaji mje mtoe elimu kwa hawa wananchi ya namna ya ugawanyaji wa rasilimali ya maji ili isifike mahali watu wanashindwa hata kuoga kwasababu maji watu wanamwagilia mashamba”. Alisema Kasilda.
Awali wananchi hao wamesema changamoto wanayokumbana nayo ya kukosa maji ya kumwagilia mashamba yao licha ya kuwa na miundombinu ya mfereji huo ni uchepushwaji wa maji kwa kutumia mipira kutoka kwenye mfereji kuelekea eneo la msala ambayo imesababisha maji kushindwa kufika kwenye mashamba ya wananchi wa Kalung'oyo jambo ambalo limewalazimu kuomba Serikali kuingilia kati kutokana na umuhimu wa mfereji huo kwenye kilimo chao.
Kwa upande wake Patrice Nyamulo, mwakilishi kutoka Bodi ya maji bonde la Pangani amesema Bodi inayojukumu la ulinzi na usimamzi wa vyanzo vya maji na kutoa kibali cha matumizi yake katika jamii, shida kubwa inayojitokeza kwenye mfereji huo ni kukosa vibali vya matumizi ya maji, hali inayopelekea kuwepo kwa matumizi holela ya maji na kusababisha uwepo wa mgogoro baina yao watumiaji maji hayo.
Aidha mfereji wa Shakaka unatoa huduma kwenye matawi matano ya Kata ya Vuje na Maore ambayo ni Kalung'oyo, Vuje, Chenona (Kata ya Vuje). Gwaya na Maweni (Kata ya Maore) yote kwa pamoja ikitegemea chanzo kimoja kikuu ambacho ni mto Hingilili unao patikana Kata ya Vuje ambao usimamizi wake upo chini ya Bodi ya maji bonde la Pangani yenye makao makuu yake Mjini Moshi.
Mwisho.
0 Comments