Header Ads Widget

CHADEMA TUNDUMA WATULIZWA NI BAADA YA KUANDAMANA WAKISHINIKIZA KUPEWA NAKALA ZA FOMU.

 


Na Moses Ng'wat,Tunduma.


MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mariam Chaurembo, amewatuliza viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika jimbo la Tunduma kwa kuwahakikishia kuwa changamoto zote zinazojitokeza katika zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa linaloendelea zitatuliwa kwa mujibu wa miongozo na hakuna mgombea atakayeenguliwa kinyume na taratibu.


Chaurembo ametoa ahadi hiyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi baada ya kukutana na viongozi wa Chadema jimbo hilo ili kuzungumzia sakata la wafuasi wa Chama hicho katika kata ya Sogea kuandamana wakilalamika kufanyiwa hujuma katika zoezi hilo.



Wafuasi hao wakiwa na wagombea wao 24 wa mitaa minne na wajummbe mchanganyiko katika kata hiyo waliandamana hadi ofisi za kata wakishinikiza kupewa nakala za fomu walizojaza kuomba kugombea, huku wakisema hawataruhusu uchaguzi ufanyike kama hawatatendewa haki.


Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo la baadhi ya wagombea hao wa Chadema kutopewa nakala ya fomu za wagombea, Chaurembo alisema suala hilo halina athari yeyote katika vigezo vinavyotumia kuteuliwa au kutoteuliwa kwa wagombea kama inavyodhaniwa na wafuasi na viongozi hao wa Chadema.


"Ni Kweli siku za hivi karibuni kuna changamoto imetokea katika kata ya Sogea iliyoripotiwa na wenzetu wa Chadema, lakini ufafanuzi ni kama huu, kwani Oktoba 26, 2024 kati ya saa tano hadi saa sita Chadema ilichuku fomu wenyeviti kwa wagombea wake wa mitaa minne na wajumbee kwa mitaa yote kasoro mtaa mmoja na kufikia saa saba mchana walirejesha fomu hizo".


"Lakini baada ya masaa manne walirudi kudai wapewe fomu waliyotakiwa kupewa kwa mujibu wa kanuni lakini muda ulikuwa umeshaisha na nikawaambia kuwa kurejesha fomu tatu sio kigezo cha wewe kuteuliwa kikubwa kinachozingatiwa ni namna gani umeijaza fomu hiyo kwa usahihi". Alifafanua zaidi Chaurembo.


Alisema walishindwa kuwapa nakala ya fomu walizokuwa wanadai kwa kuwa wao ndio waliorudisha fomu zote tatu badala ya mbili kama kanuni zinavyotaka na tayari zimehifadhiwa kwenye chumba mahususi hivyo kitendo cha kuanza kuzitafuta kule zilikohifadhiwa ni sawa na kuanza zoezi la uchambuzi kabla ya muda wake.


Aidha, Chaurembo aliwataka viongozi wa vyama vya siasa vinavyosimamisha wagombea kuamini kuwa zoezi hilo linafanyika kwa haki na baada ya kukamilika majina ya wagombea wote yatabandikwa na kutakuwa na muda wa kuweka mapingamizi na changamoto zitakazobainika.



Awali, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Tunduma, Boniface Mwakabanje, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kata ya Sogea ambapo wafuasi na wagombea wa chama hicho walikusanyika wakishinikiza kupewa nakala ya fomu za wahombea, alisema suala la wagombea kupewa nakala ni suala la muhimu.


"Hatutaki kufanya makosa kama chaguzi zilizopita na imekuwa ikitumika mianya hii sisi kuenguliwa kwenye chaguzi na tunataka uchaguzi huru na haki na hatuko tayari kuachia uchaguzi huu na CCM hawapaswi kutumia ujanja kushinda " alisema Mwakabanje.


Hadi kufikia sasa zoezi la uchukuaji na urejeahaji wa fomu katika Halmashauri ya Mji Tunduma  limefikia asilimia 90, huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kimechukua fomu kwenye mitaa yote 71 na Chadema tayari ilikuwa imechukua kwenye mitaa 60.


Halmashauri ya Mji Tunduma ina jumla ya  mitaa 17 na kata 15, huku vituo vya wapiga kura vikiwa 196.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI