Na Thobias Mwanakatwe,KOROGWE
WAGONGWA wa macho 34,488 waliokosa huduma za kibingwa za matibabu ya macho wamepatiwa matibabu bure kupitia ufadhiri wa Taasisi ya Mo Dewji Foundation iliyotolewa katika mikoa sita nchini.
Kati ya wagonjwa hao, 2,327 waliokuwa wakisumbuliwa matatizo mbalimbali ikiwamo mtoto wa jicho,uvimbe wa nyama kuota kwenye jicho wamefanyiwa upasuaji.
Mratibu wa Miradi ya Taasisi ya Mo Dewji Foundation, Amina Ramadhani, alisema hayo juzi wakati wa zoezi la utoaji huduma za matibabu ya magonjwa ya macho kwa siku tatu yakiyokuwa yakifanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Alisema wagonjwa hao wameonwa katika kambi zilizofanyika kwa muda wa miezi nane katika mikoa ya Singida, Lindi, Dodoma, Mtwara, Morogoro na Tanga.
Ramadhani alisema katika kipindi hicho pia wagonjwa wa macho 14,509 walipewa miwani bure ya kusomea na wengine 21,760 walipewa dawa za macho.
"Kambi za matibabu ya macho kwa Mkoa wa Singida zilifanyika Manispaa ya Singida, Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Dodoma ilifanyika Wilaya ya Kondoa,Mtwara Masasi, Morogoro ilifanyika katika Wilayanya Ifarakara wakati kwa Mkoa wa Tanga huduma zilifanyika katika Wilaya ya Muheza,Manispaa ya Tanga na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe," alisema.
Alisema kuwa Taasisi ya Mo Dewji Foundation imejiwekea malengo katika kipindi cha mwaka mmoja iweze kuwafikia wananchi 50,000 kuwapatia bure huduma za matibabu ya kibingwa ya macho hususani wasiokuwa na uwezo.
Naye Daktari wa Macho, Salim Mohamed, alisema idadi kubwa ya wagonjwa katika kambi walizofanya inatokana na wananchi kuwa mbali na huduma za kibingwa za macho zinakotolewa.
Alisema tatizo la mtoto wa jicho ambalo wagonjwa wengi wamegundulika kuwa nalo linatokana na umri mkubwa,kuumia na kuwa na presha au ugonjwa wa kisukari.
Hadi zoezi kutoa matiba linahitimishwa katikaHalmashauri ya Wilaya ya Korogwe wagonjwa 4,228 walionwa, 376 walifanyiwa upasuaji, 1999 walipewa miwani ya macho na wagonjwa 2790 walipewa dawa.
0 Comments