Header Ads Widget

WAFANYABIASHARA RUVUMA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA FURSA YA TAMASHA LA UTAMADUNI



Na Elizabeth Zaya 


KUFUATIA Tamasha la Utamaduni la Taifa kupelekwa mkoani Ruvuma, baadhi ya wakazi mkoani humo wamefurahia na kuelezea namna ambavyo wamejipanga kunufaika nalo kupitia fursa mbalimbali zitakazopatina katika kipindi chote ambacho litafanyika mkoani kwao.


Pia wamemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwa na tamasha la utamaduni kwa kuwa pamoja na kuwakumbusha kuenzi tamaduni zao lakini wanalitumia kujinufaisha kiuchumi.



Tito Mbilinyi, mkazi wa Songea mkoani Ruvuma, anasema kwamba matamanio yao kwa miaka mingi ilikuwa kuona tamaduni zao zinaendelezwa, hivyo wanampongeza Rais Samia kwa kuliona hilo na kuruhusu kufanyika.



“Mimi namshukuru sana Rais Samia kwa kutuletea tamasha hili, tulilisubiri sana, kwa hiyo tunashukuru sana. 



Sisi kama wafanyabiashara tunasema hivi, karibu mgeni, mwenyeji apone, kwa sababu hata mwenye nyumba ya kulala wageni, mama lishe, anayejishughulisha na usafirishaji,wote tutanufaika kwa sababu ugeni utakaokuja ni mkubwa sana,”amesema Mbilinyi.



“Na haya ndiyo tulikuwa tunaomba miaka yote kwamba angalau viongozi wetu wa mkoa wawe wanatuletea fursa kama hizo, sisi tunasema tunampongeza sana Rais Samia, kwanza ametuelewa sana sisi sekta binasfi hasa katika biashara na nimsikivu kwa sababu  zile changamoto ambazo tumekuwa tukizilalamikia kwa miaka mingi naona ameanza kuzitatua, tunamshukuru sana.”



Anasema wakazi wa mkoa huo wamefurahi na wanamsubiri kumpokea Rais Samia mkoani kwao na wamejipanga kumuonyesha utajiri uliopo  katika mkoa huo.


“Rais wetu tunamkaribisha mkoa wa Ruvuma, sisi ni wenyeji na wakulima wa mahindi na tunajidai kwa sababu tunalisha mikoa mbalimbali yenye shida ya chakula pamoja na nchi za nje, kwa hiyo tunamkaribisha mama yetu kwenye mkoa wetu wa chakula angalau atakapoondoka tutampatia na yeye mahindi akale nyumbani,”anasema Mbilinyi.


Upendo Mwakikapwa anaema wao kama wafanyabiashara, wamejipanga vya kutosha kupokea na kuhudumia ugeni utakaofika mkoani kwao katika kipindi chote cha tamasha na kwamba watahakikisha wanatoa huduma zote zitakazohitajika kwa ubora.


“Baada ya kupata taarifa kwamba Rais Samia atatembelea mkoani kwetu wakati wa tamasha la utamaduni, tulianza kujipanga na mpaka sasa naweza kuwahakikishia wageni wote watakaofika kwamba tuko tayari kuwapokea na kuwahudumia,”amesema Upendo.


“Na tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wageni wote watakaofika kwenye mkoa wetu wanapata sehemu za kulala bila shida, wanapata chakula na huduma nyingine muhimu zitakazohitajika, na tunaamini na sisi wafanyabiashara na mwananchi mmoja mmoja tutanufaika, kwa hiyo tunashukuru kwamba hizi pilika zilizopo kwa sasa kutokana na ujio wa Rais Samia inasaidia kukuza uchumi kwa wakazi wa mkoa huu.”


Upendo anampongeza Rais Samia kwa kazi ambayo ameifanya katika mkoa wao huo wa Ruvuma katika Nyanja mbalimbali ikiwamo uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambayo imerahisisha kwa kiwango kikubwa ufanyaji wa biashara na kuchochea kukuza uchumi wao.


Anasema tofauti na miaka ya nyuma, kwa sasa mkoa huo unazidi  kukua kiuchumi kutokana na shughuli nyingi zinazofanyika humo ikiwamo zile za uchimbaji wa makaa ya mawe ambao umesababisha pia shughuli za usafirishaji kuongezeka.


“Kwa hiyo hata Rais akija atashuhudia hizi pilika zilizopo na kikubwa tunamshukuru sana kwamba amechangia kwa kiwango kikubwa shughuli za kiuchumi kuongezeka katika mkoa huu kwa sababu ya kuimarisha miundombinu ya barabara, na hata viongozi wanapofika namna hii, fursa zinaongezeka zaidi kwa hiyo tunamshukuru sana kwa kuuona na kuuthamini mkoa wetu,”anasema Upendo.“


Tunamwambia Rais Samia kuwa, tunamsubiri na tunamkaribisha kwa mikono miwili na akifika atafurahi mwenyewe namna ambavyo tumejipanga kumpokea, na kutokana na yale aliyoyafanya katika mkoa wetu tumeandaa mapokezi ambayo yatamshawishi kurudi tena kwa mara nyingine.”


Anasema wafanyabiashara wote na wafanyabiashara wa mkoa huo, wanafurahia ujio wa Rais Samia na wamepanga kumwambia neno la shukrani kwa mambo ambayo amewafanyia.


“Kwa hiyo ujio wa Rais Samia sisi tumeupokea kwa furaha kubwa, ni mkubwa kwa sababu utatuachia fursa kubwa, kitendo cha watu kusafiri kutoka sehemu mbalimbali na kuja katika mkoa wetu, sisi tunatakiwa tujiongeze, kutoka moyni mwangu mimi kama mwanamke, ninamkaribisha sana Rais wetu na wanawake wa mkoa huu tupo tayari kumpokea na hii ni neema kwetu,”anasema Upendo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI