Picha hii ya mtandaoni haihusiani Moja kwa Moja na habari hii
Na ABDALAbdallah Amiri Igunga
Katibu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM ) Tawi la Ibole Kijiji cha Ibole Kata ya Igurubi wilayani Igunga mkoani Tabora, Juma Nzera, anadaiwa kuuawa baada ya kushambuliwa na jeshi la jadi (sungusungu) kisha mwili wake kuutupwa kichakani.
Akizungumza mmoja ya wananchi wa kijiji hicho, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Jiganga Jilunga alisema tukio hilo lilitokea September 13, mwaka huu ambapo akiwa anachunga ng’ombe walinzi hao wa jadi zaidi ya 400 wakiwa na mikuki, pinde, fimbo na malungu wakitokea kijiji cha Ngofila kilichopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga walimvamia na kuanza kumshambulia.
Alisema baada ya saa 3 sungusungu hao walirudi kuelekea kijijini kwao wakiwa wamemtanguliza Katibu wa Tawi, Juma Nzera ambaye kwa sasa ni marehemu.
"Nilijaribu kuwauliza kulikoni katibu wetu anachukuliwa bila taarifa, nilijibiwa kuwa nisirudietena kuuliza swali hilo vinginevyo nitashughulikiwa.
Mtendaji wa Kata ya Igurubi, Michael Kasitu alidhibitisha kuuawa kwa katibu huyo ambapo alisema:
"Nikweli kiongozi huyo ameuawa na watu wanaodaiwa kuwa ni sungusungu wa kijiji cha Ngofila wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga."alisema mtendaji huo.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Igunga, Peter Olonge alikiri kuuawa kwa katibu huyo na kusema kuwa chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana kwa kuwa sungusungu wa kijiji cha Ngofila wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga walikuja hadi kijijini kwake na kumchukua pasipo kujua kosa lake.
Hata hivyo, Olonge alisema marehemu katika uhai wake hajawahi kuhisiwa kwa kosa lolote wala hajawahi kujihusisha na vitendo vya uharifu na alikuwa mchapakazi mwaminifu kwa chama chake na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alikiri kupokea taarifa hizo za mauaji ya katibu huyo wa tawi wa CCM.
"Ni kweli tukio hilo lipo, lakini siwezi kulizungumzia kwa kuwa katibu aliyeuawa walimuulia wilaya ya Kishapu, hivyo anayepaswa kulizungumzia suala hilo ni uongozi wa Mkoa wa Shinyanga”.
Mwisho.
0 Comments