Mkuu wa wilaya Kigoma Salum Kali (katikati) kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye akizindua kitabu cha historia ya mkoa Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye ametoa wito kwa wananchi wa mkoa Kigoma kutumia uwepo wa kitabu cha historia ya mkoa Kigoma kukuza Kiswahili sambamba na kufundisha mil ana desturi za wananchi wa mkoa huo.
Andengenye alisema hayo akizundua kitabu kilichoandikwa na Mwandishi wa Habari na Mwandishi wa vitabu, Shomari Hamisi kinachoeleza kuhusu mambo mbalimbali ya mkoa Kigoma ikiwemo historia za watu, viongozi, makabilia, uchumi na masuala ya mila na desturi.
Mkuu huyo wa mkoa Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali alisema kuwa kitabu hicho kimewashirikisha viongozi na wasomi mbalimbali kutokana na utafiti uliofanywa hivyo amewataka wananchi wa mkoa huo kukitumia kitabu hicho kama rejea.
Akisoma risala ya uzinduzi wa kitabu hicho Mshauri wa kamati iliyosimamia uzinduzi wa kitabu hicho,Dk.Hamimu Hongo alisema kuwa wakati mwingine yapo mambo yaliyokuwepo ambayo hayafahamiki lakini yapo mambo mapya yanaendelea kugunduliwa hivyo kitabu hicho kinayo mambo mengi ya mkoa Kigoma ambayo bado watu wengi hawayajui.
Alisema kuwa chimbuko la utunzaji wa kitabu hicho ni kuona mkoa Kigoma ukiwa na historia kubwa iliyotukuka lakini haijaandikwa mahali popote na hivyo kumfanya mwandishi kufanya kazi kubwa ya utafiti na kupata msaada wa watu mbalimbali ikiwemo ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na kufanikisha kitabu hicho kuandikwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mwandishi wa kitabu hicho,Shomari Hamisi alisemaa kuwa kilichompa msukumo wa kuandika kitabu hicho ni chachu ya mambo makubwa yaliyomo mkoani humo lakini yanaandikwa kwa kudonolewa na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Hamisi alisema kuwa ilimchukua miaka saba ya kukusanya rasimu, nyaraka na kufanya mahojiano na watu mbalimbali historia iliyoanza kabla ya uhuru maana walikuwepo watu wakiishi huko na baada ya uhuru.
0 Comments