Na Thobias Mwanakatwe,MKALAMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Asia Messos, amewataka wananchi wilayani humo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.
Ametoa wito huo jana wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa vijiji vya Gumanga na Nduguti wilayani hapa
“Nawasihi msipoteze haki zenu za msingi, utakapofika wakati wa kujiandikisha, mjiandikishe, utakapofika wakati wa kampeni jitokeze na itakapofika wakati wa kupiga kura tujitokeze kuwachagua viongozi wetu tunaowataka,” alisema.
Akizungumzia suala la maadili, Messos amewakumbusha wakazi wa vijiji vya Nduguti na Gumanga kuwa mstari wa mbele kupinga mila na desturi zinachochea mmomonyoko wa maadili katika jamii.
“Tujikite sana katika malezi yetu, turudi katika misingi yetu ya kitanzania. Hii iwe ajenda kubwa katika mikutano yetu, katika nyumba zetu za ibaada. Tuungane pamoja kupinga ushoga na usagaji katika jamii zetu,” alisema Messos
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Mkalama amewataka wazazi wilayani hapa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kwa manufaa ya maisha ya baadae pamoja na kusisitiza suala la kuchangia chakula shuleni.
Awali akielezea mambo makubwa yaliyofanywa na serikali katika miaka 3 ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Messos alisema Halmashuri ya wilaya ya Mkalama imepokea zaidi ya Sh. Bilioni 60 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya elimu,afya umeme,barabara pamoja na kilimo.






0 Comments