Na Mariam Kagenda_Kagera
Wapiga kura wapya Milioni 5,586,433 Nchini wanatarajia kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi Nchini Tanzania sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020.
Taarifa hiyo imetolewa na mwakilishi wa mkurugenzi wa uchaguzi kutoka Tume huru ya Taifa ya uchaguzi Bi.Giveness Aswile wakati wa mkutano wa tume ya taifa ya uchaguzi na wadau wa uchaguzi mkoa wa Kagera kuhusu uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura.
Bi Giveness amesema kwa mkoa wa Kagera wapiga kura wapya wanaotarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari hilo ni 219,321 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.5 ya wapiga kura 1,412,008 waliopo kwenye Daftari ambapo Tume huru ya Taifa ya uchaguzi inatarajia baada ya uandikishaji mkoa wa Kagera utakuwa na wapiga kura 1,631,329 na kwa mkoa huo zoezi la uboreshaji wa Daftari utaanza tarehe 5 mpaka 11 mwezi wa 8
Amesema idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/2020 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura kwa sababu mbalimbali hawakuweza kujiandikisha .
Ameongeza kuwa zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi pamoja na wale watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025,kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na wamehama ili waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au Jimbo walipoandikishwa awali , kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na waliofariki.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini (INEC) Makamu mwenyekiti wa tume hiyo Mbaruku.S. Mbaruku Jaji mstaafu wa mahakama ya rufani amewataka wadau wa tume hiyo mkoa wa Kagera kusaidia Tume katika uhamasishaji kwa walengwa wa zoezi hilo ili mkoa wa Kagera utakapoanza zoezi hilo waweze kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
0 Comments