NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Wananchi wa kijiji cha Sanje kata ya Santilya wilayani Mbeya wanakabiliwa na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kituo cha afya Santilya kutokana na kijiji chao kutokuwa na zahanati.
Wakizungumza na kituo hiki kijijini kwao wananchi hao wamesema hawana zahanati hivyo hulazimika kusafiri kwa tabu kwa umbali wa kilomita zaidi ya sita kwenda makao makuu ya kata kufuata huduma za afya na hivi karibuni walilazimika kuanza ujenzi wa zahanati kwa nguvu zao mbaya zaidi barabara ni mbovu kwenda kituo cha afya.
Kwenye mkutano wa hadhara kati ya wananchi wa Sanje na Mbunge wa Mbeya vijijini baada ya kufika kijijini hapo, Diwani wa kata ya Santilya Mwawa Jimson Mwaluanda, amesema kutokana na kadhia hiyo kwa muda mrefu wananchi wamejenga zahanati kwa kukamilisha majengo mawili makubwa hadi kupaua na kuomba ushiriki wa Serikali.
Oran Njeza ndiye Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini amezungumza na wananchi hao na kuwapa pole kwa adha na kueleza kuwa lengo la Serikali ni kuimarisha vituo vya afya kuwa vya kimkakati na kuboresha barabara ili zipitike kwa urahisi na kuahidi kuwaunga mkono wana Sanje kwenye ujenzi wa zahanati yao.
Baada ya kijiji cha Sanje Mbunge Njeza akaelekea kijiji cha Itizi ambako Ofisa mipango kutoka Halmashauri ya Mbeya Bi. Beatrice Keffa Urio ameona juhudi za wananchi wa kijiji cha Sanje na Itizi na kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo anasema Serikali itakamilisha hatua zinazohitajika hivyo kuutaka uongozi wa kata kuwasilisha mahitaji Halmashauri.
Mbunge wa Mbeya vijijini anaendelea na ziara katika Jimbo lake akiendelea kukutana na wananchi wake na kusikiliza kero zao huku akieleza mambo ambayo tayari yametekelezwa, inayoendelea kutekelezwa na mipango ya usoni juu ya miradi inayotarajiwa kutekelezwa.









0 Comments