NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Baada ya kumaliza vikao vya bunge la bajeti, Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, ameanza ziara katika Jimbo hilo kwa kutembelea shule ya msingi Izumbwe II kata ya Iwiji.
Akiwa shuleni hapo Mbunge Oran Manasse Njeza amepokea kero kadhaa kutoka kwa watumishi wa shule hiyo ikiwemo uchakavu wa vyumba vya madarasa kiasi cha baadhi kuwa na nyufa hali ambayo ni hatari kwa usalama wa watoto hao wa elimu ya msingi.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Izumbwe II Ipyana Wilson Ndumba, amemwambia Mbunge huyo kuwa shule hiyo ilianza zaidi ya miaka hamsini iliyopita na miundombinu yake ni chakavu hivyo kuiomba Serikali kuitazama shule yake hiyo ili watoto kusoma kwenye mazingira safi na salama na kuongeza ufaulu.
Mbunge Njeza, amepokea kadhia hiyo baada ya kutembelea vyumba vyote vya madarasa shuleni hapo na kujionea ubovu na uchakavu wa baadhi ya vyumba, upungufu wa ofisi za walimu na upungufu wa watumishi hasa wakike na ukosefu wa huduma ya maji shuleni hapo.
Mbunge Oran Njeza ameiomba ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya kwenda kuangalia namna ya upatikanaji wa fedha ili kuinusuru shule hiyo kongwe na kuinua ufaulu wa watoto.
Akizungumza na watumishi, wanafunzi na ujumbe aliyoambatana nao, Njeza amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuahidi kwa kila mwanafunzi wa darasa la saba atakayepata ufaulu wa alama A atapewa zawadi ya shilingi laki moja.
Sanjari na hayo Mhe. Mbunge ameahidi wahusika kutembelea shule hiyo ili kufanya tathmini ya kuikarabati ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo kongwe ambayo iko pembezoni mwa Jimbo, wilaya na inapakana na wilaya ya Ileje mkoani Songwe huku kuhusu upungufu wa madawati akiitaka Halmashauri ya kijiji kutafuta miti na mashine ili atoe mafuta ya disel kwa ajili ya kupasua mbao na kutengenezea madawati sitini yanayohitajika kwa watoto hao.









0 Comments