Header Ads Widget

MJENGWA ACHAMBUA MSIGWA KUHAMA CHADEMA

 


Tafakuri Jadidi:

Kwamba Msigwa Ni Bayaye…


Afrika safari ya mwanasiasa yaweza kuwa ngumu.

Kwenye safari ya kisiasa ya Mchungaji Peter Msigwa hatimaye leo imeripotiwa ametua CCM.


Tafsiri yake?


Kwamba kwa kumtafakari Msigwa, anatutaka tufikiri, kuwa CCM sio tu kihistoria ni kimbilio la wanyonge, bali, ni kimbilio pia la baadhi ya wanasiasa wa upinzani walio safarini na katikati ya mahangaiko ya kisiasa.


Msigwa ameelezea tabu alizokumbana nazo ‘ safarini’ inapohusu demokrasia ya ndani ya chama alichokikimbia. Kwamba kuna shida kwenye eneo hilo, Intra-party democracy, wanasema kwa kimombo.


Kwamba Msigwa ni Bayaye, je, Afrika Bayaye ni nani?


Jibu:


Afrika kuna viongozi wanasiasa wa aina tatu;


1. Wenye kutokea kwenye koo za kisiasa

2. Wenye kutokea kwenye familia za kitajiri au wa kipato cha kati

3. Wenye kutokea kwenye familia za kawaida na hata masikini.


Tangu siku ya kwanza, Afrika  kijana anayeingia mjini kutoka kijijini na kuishi akihangaika kuhemea kwa kazi za vibarua au biashara za uchuuzi, basi, hugeuka kuwa Bayaye.


Hata kwa waliozaliwa mijini lakini kutoka kwenye vitongoji vya kaya masikini, nao hugeuka kuwa Ma-bayaye.


Ndivyo walivyokuwa wakijulikana katika nchi ya Uganda. Na miji mingi ya Afrika ya sasa imefurika ma-bayaye. 


Mabayaye Afrika wana sifa ya upambanaji- hustlers. Wengine huchomoka kwenye kundi na kuwa na mafanikio makubwa sana.


Yumkini Peter Msigwa ametokea kwenye kundi hili. Nilikutana kwa mara ya kwanza na Peter pale Iringa mwaka 2004. 


Peter, kama nilivyozoea kumwita,  alikuwa msomaji wa makala zangu gazetini na tukawa marafiki tangu hapo. 


Peter niliyemjua, hata kabla ya kuwa chochote ndani ya Chadema alikuwa ni mpambanaji katika kujitafutia kipato hata akaniambia siku moja, kuwa ameanzisha biashara ya kuuza maua. 


Kwa historia yake ya kimaisha amewahi hata kuuza mitumba. Hiyo ni tafsiri sahihi ya Bayaye. Uzuri wa Peter Msigwa haionei aibu historia yake.


Peter Msigwa niliyemjua alikuwa mahiri pia kwenye ujenzi wa hoja za kisiasa. Aliishi eneo la Gangilonga jirani na nilikoishi. 


Mara kadhaa ilitokea tukatembea pamoja kwa miguu kutoka katikati ya mji wa Iringa kurudi makwetu. Njiani stori zilikuwa za masuala ya siasa tu. 


Nilimwona mapema, kuwa mbali ya kujiingiza kwenye uchungaji, Peter angekwenda kuwa mwanasiasa. Kwamba alianzia kwenye upinzani haikunishangaza pia. Na kwamba sasa amehamia CCM haitamchukua muda mrefu kwa Peter kulizoea koti la CCM na itikadi zake. Hata akiwa Chadema, Peter ameifuatilia kwa karibu sana CCM.


Nakumbuka matukio mawili Peter Msigwa akiwa Chadema;

Mosi, siku ile nilipokutana nae Dodoma akiwa ametoka kuapishwa kama Mbunge mpya wa Chadema jimbo la Iringa Mjini. Ni mwaka 2011. 

Nilitokea Singida kwa kazi zangu na nikapita Dodoma kuelekea nyumbani Iringa.


Nikamwona Peter Msigwa akitembea kwa miguu kwenye viunga vya mji wa Dodoma jirani na kituo cha mafuta. Ni kumbukumbu ya picha hiyo niliyompiga pale Dodoma kwa mara ya kwanza na akiwa Mbunge wetu wa Iringa Mjini.


Tulisimama wima tukiongea huku wenyeji wa mji wakitupita bila kumtambua kuwa ni Mbunge Msigwa. Akaja kuwa maarufu sana ndani na nje ya Bunge.


Tukio jingine ni pale nilipopata ugeni wa Afisa wa Ubalozi wa Finland aliyetaka pia kufika kuongea na wanafunzi wa  Journalism Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa. 


Nikampigia simu Mheshimiwa Mbunge Msigwa kumwomba ashiriki tukio hilo na aongee machache. 

Mbunge Msigwa hata kwa taarifa ile ya muda mfupi, na bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na wakati mwingine misimamo, aliitikia wito na akaja kushiriki tukio.

Kila la Heri Peter!

Maggid,

Zanzibar.

PS:

Peter sasa azoee kuweka mfukoni kalamu ya rangi ya kijani, siyo hiyo ya buluu!

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI