Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MBUNGE wa jimbo la Kigoma Kaskazini Asa Makanika amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan imedhamiria kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi na kubadilisha hali zao za kiuchumi kufuatia kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kijamii ambayo inagusa Maisha ya wananchi wa jimbo hilo moja kwa moja.
Makanika alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhra katika Kijiji cha Milinzi Tarafa ya Kalinzi jimbo la Kigoma Kaskazini wilaya ya Kigoma ambapo amesema kuwa Pamoja na hivyo ametaka taasisi zinazopewa fedha na serikali kwa ajili ya utekelezaji miradi kuhakikisha miradi hiyo inafika vijijini kwa wananchi na inatoa huduma.
Akizungumza katika mkutano huo Makanika alisema kuwa Raisi Samia ameonyesha nia ya dhati katika kuwahudumia wananchi hao ambapo ameeleza kutekelezwa kwa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo vituo vitatu vimejengwa katika jimbo kwa kipindi cha miaka mitatu, shule 12 za sekondari, kumalizika kwa ujenzi wa hopsitali ya wilaya iliyogharimu shilingi Bilioni 3.5 huku miradi ya umeme vijijini (REA) ikipelekwa hadi kwenye vitongoji sambaamba na kuimarishwa kwa bara bara za vijijini kusaidia usafirishaji wa mazao.
Pamoja na hilo Mbunge huyo akiwa kwenye mikutano hiyo amewataka watendaji kutoka TARURA,TANESCO, RUWASA na mamlaka za serikali zinazosimamia utekelezaji wa miradi katika jimbo hili kutekeleza majukumu yao kwa kutumia utaalam wao na kuhakikisha miradi inakamilika na wananchi wananufaika na kukamilika kwa miradi hiyo huku akieleza mfuko wa jimbo kuchangia milioni 81 katika kuchochea utekelezaji wa miradi hiyo .
Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma, Elius Mutapima alisema kuwa juhudi za wabunge akiwemo mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kaskazini zimewezesha serikali kuongeza bajeti maradufu ya miradi ya barabara ikiwemo wilaya ya Kigoma ambapo kwa sasa imepata kiasi cha shilingi Bilioni 2.2 kutoka milioni 400 miaka miwili iliyopita.
Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya REA kwenye wilaya ya Kigoma Mhandisi wa TANESCO anayesimamia miradi ya umeme vijijini katika wilaya hiyo, Joseph Kanje alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa miradi hiyo kutokana na kuchelewa kupatika kwa fedha lakini kwa sasa miradi kwenye wilaya hiyo itaanza mwishoni mwa mwezi huu na umeme utafika kwenye vitongoji vyote vya jimbo hilo.
0 Comments