Header Ads Widget

KASI YA MAENDELEO KATA YA NJIAPANDA YAWAKOSHA WANANCHI, WAMPA ZAWADI RAIS SAMIA NA MBUNGE KIMEI

 


Na WILLIUM PAUL, MOSHI.


KATIKA kipindi cha mwaka 2021 hadi sasa kata ya Njiapanda imefanikiwa kupata miradi lukuki ya maendeleo kama vile mradi mkubwa wa maji toka Miwaleni wa shilingi bilioni 2.3, sekondari mpya shilingi milioni 600, shule mpya ya msingi Darajani shilingi milioni 348.


Mradi mwingine ni zahanati mbili za Njiapanda shilingi milioni 115 na Kilema Pofo shilingi milioni 50, matundu ya vyoo na ukarabati wa shule za Njiapanda na Dkt. Shein pamoja na mradi wa ukwekaji uzio na ujenzi wa vyoo vya kisasa mnada wa mifugo Njiapanda shilingi milioni 45.



Mafanikio haya yamewasukuma wananchi wa kitongoji cha Njiapanda Mashariki eneo la Otomoro kumpa zawadi maalum Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt Charles Stephen Kimei pamoja na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliyovikwa katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Samwel Mahanyu kwa niaba yake. 


Dkt Kimei amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani mabilioni ya fedha katika miradi mbalimbali jimboni humo ni matokeo ya moyo wake wa upendo na utayari wake katika kuwatumikia wananchi ndio maana serikali anayoiongoza imekuwa ikitekeleza miradi ambayo inalenga mahitaji ya watu kitu ambacho ni matumizi mazuri ya kodi za wananchi. 



Mbunge Kimei ameeleza hayo wakati akiendelea na ziara yake Jimboni ambapo amekuwa kata ya Njiapanda alipokagua miradi na kuzungumza na wananchi wa Otomoro, Njiapanda Mashariki. 


Katika mkutano huo ameeleza pia mpango wa matengenezo ya barabara katika mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo kata ya Njiapanda ikiwemo ya takribani kilomita 50.



Vile vile Dkt Kimei amesema mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika kata hiyo utaendelea katika mwaka huu wa fedha hali itakayoufanya mji huu unaokua kwa kasi kujengeka katika namna bora na kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya viwanda, makaburi, makazi na biashara. 


Aidha amewatoa hofu wananchi wanaosubiri fidia kupisha eneo la ujenzi wa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa mizigo eneo la Ghona na Njiapanda kwamba watalipwa fidia katika mwaka huu wa fedha 2024/25. 



Dkt Kimei amewaomba wenyeviti wa vitongoji kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili visaidiane na jeshi la polisi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. 


Pia kupitia mkutano huo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira amewahakikishia wananchi wa eneo hilo kwamba mpaka mwezi Disemba, 2024 hakutakua na tatizo la kukosekana kwa maji katika eneo hilo kwa kuwa watatekeleza mradi wa maboresho wa kilomita 8. 



Naye Katibu wa CCM amesema siasa ni maendeleo sio porojo na propaganda na kusisitiza kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi inayoonekana kila kata katika Jimbo la Vunjo ni matunda ya kuwa na Mbunge asiyesusia vikao vya Bunge na ambaye kila fursa anayoipata ndani na nje ya Bunge anasemea mahitaji ya Jimbo na wananchi waliomtuma hivyo akawataka wananchi wasifanye makosa tena. 


Mahanyu amesema wananchi wanaelewa kazi ya maendeleo ni kazi ya CCM hivyo kazi kubwa iliyofanyika ni turufu muhimu ya ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 hapo mbeleni.



Ziara hiyo walishiriki wajumbe wa kamati za siasa Kata ya Njiapanda, wataalam Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Wilaya ya Moshi Vijijini Andrew Mwandu, Katibu wa UWT Wilaya Moshi Vijijini Shakila Singano pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Emanuel Mlaki.


Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI