Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amehudhuria katika mahafali ya Ishirini na mbili (22) ya Taasisi ya Mafunzo ya Afya na Sayansi Shirikishi Kibosho yenye kauli mbiu "Elimu ya Afya ni msingi wa mafanikio na mabadiliko".
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 56 walipewa vyeti ngazi ya Stashahada (Diploma), 47 wakiwa katika fani ya Uuguzi na Ukunga, na 7 katika fani za Afya ya Mdomo na Meno.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi Padri Dkt. Reginaldi Sipendi, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi, Shally Raymond ambaye pia ni Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Kilimanjaro, Mfanyabiashara kutoka Dar es Salaam, Martin Mbwana Massawe, Wazazi/Walezi wa wahitimu, na wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaoendelea na Mafunzo katika Taasisi hiyo.
Awali, akisoma ibada kabla ya sherehe za Mahafali hayo, mwakilishi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi Padri Dkt. Reginald Sipendi aliwaasa vijana kumtanguliza Mungu mbele wanapokwenda kuanza majukumu yao na kuwataka kuwa na Huruma, Wema, Upendo na Unyenyekevu wanapohudumia wagonjwa.
Wakisoma risala kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Taasisi hiyo Devota Shayo na wahitimu walieleza kuwa changamoto kubwa zinazowakabili ni pamoja na uhaba wa madarasa ya kufundishia, ukosefu wa umeme mbadala pindi umeme wa TANESCO unapokatika, uhaba wa vifaa vya kufundishia kama vile projector, vitabu na komputa, pamoja na uhaba wa viti.
Mkuu wa Taasisi alimuomba mgeni rasmi kuwasaidia kutatua changamoto zote alizoelezwa kwenye risala zao kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Akiongea na wahitimu, wakufunzi, wazazi/walezi pamoja na wageni waalikwa, mgeni rasmi, Ndakidemi aliushukuru uongozi mzima wa Taasisi kwa kumshirikisha katika hafla hiyo.
Alisema, kutokana na uwepo wa hospitali ya Kibosho na mazingira mazuri ya kufundishia, alishauri ni vyema Taasisi hiyo ikapandishwa hadhi ili watoe Shahada ya Uuguzi na Ukunga na ile ya Afya ya Mdomo na Meno kwani nchi ina uhitaji mkubwa wa wataalamu kutoka katika fani hizi.
Akijibu changamoto alizoelezwa katika risala zao, mgeni rasmi aliiomba Taasisi iandae BOQ itakayoainisha gharama za kujenga madarasa pamoja na jenereta ya kuzalisha umeme.
Mfanyabiashara wa Dar es salaam Martin Massawe alijitolea kusaidia vyombo vya TEHAMA (projector na computer) vinavyohitajika.
Ndakidemi aliwaomba wageni waliokuwepo katika mahafali hayo wajitoe kwa hali na mali ili kukabiliana na changamoto ya viti.
Katika harambee iliyoendeshwa, zilipatikana shilingi milioni 3 taslimu na laki mbili ahadi huku Mbunge Ndakidemi alitoa kiasi cha shilingi milioni mbili taslimu kama mchango wake wa kununua viti.
Wengine waliochangia viti kwa kutoa pesa taslimu ni pamoja na Shally Raymond (350,000) na Martin Massawe (250,000).
Akitoa shukrani zake, Mkuu wa Taasisi Devota Shayo alimshukuru sana Mbunge kwa kukukubali kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya wahitimu wa Taasisi yao.
Mwisho..
0 Comments