Na Fadhili Abdallah,Kigoma
DIWANI wa kata ya Kitongoni Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma Himidi Omari amepongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa iliyofanya kwenye kata hiyo na kuwezesha kupelekwa kwa kiasi cha shilingi Bilioni 18 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi maendeleo ya wananchi wa kata hiyo na mkoa Kigoma kwa jumla.
Himidi hayo akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kwenye soko la zamani la Watumwa Ujiji alisema kuwa Raisi Samia ni Mwanamke lakini amefanya makubwa ambayo baadhi ya wanaume hawawezi kufanya na kusema kuwa fedha hizo zimeleta maendeleo na mabadiliko makubwa ya madhari na kuinua uchumi wa wananchi wa kata hiyo.
Alitaja moja ya miradi hiyo kuwa ni uboreshwaji wa bandari ya Ujiji ambayo inatumika kwa ajili ya boti za abiria na mizigo zinazofanya safari zake ndani ya ziwa Tanganyika na hivyo kurahisisha upakiaji na upakuaji wa shehena kwenye bandari hiyo.
Diwani huyo wa kata ya Kitongoni alitaja miradi mingine kuwa ni Pamoja na ujenzi wa machinjio ya Ujiji iliyogharimu shilingi milioni 400, milioni 310 kwa ajili ya vyumba 12 vya madarasa na madawati 160 kwa shule ya sekondari Kitongoni, ujenzi wa zahanati mpya katika kata hiyo iliyogharimu shilingi 130 na shilingi milioni 500 kwa ujenzi wa barabara ya kiwango cha zege katika mtaa wa Mnazi Mmoja.
Akizungumza katika mkutano huo ulioenda sambamba na uzinduzi la Tamasha la kila mwaka la Samia Festival linaloandaliwa na diwani wa kata hiyo ya Kitongoni, Naibu Waziri TAMISEMI,Zainab Katimba alisema kuwa serikali itaendelea kuleta fedha kugharamia miradi mbalimbali ya wananchi kwa ajili ya kuondoa lakini pia kuleta maendeleo ya wananchi.
Alisema kuwa kwa miaka hii mitatu serikali ya Raisi Samia imeshusha kiasi cha shilingi Trilioni 11.9 kwa mkoa Kigoma pekee kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kutoa huduma lakini kwa ajili ya kuinua shughuli za uchumi za wananchi wa mkoa Kigoma.
Mwisho.
0 Comments