Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Njombe wamejitokeza katika mazishi ya mfanyabiashara Godfrey Ndambo aliyefariki kwa kuuawa na watu wasiofahamika nje ya geti la nyumba yake huko Uzunguni Ramadhani huku Chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Njombe kikiiagiza serikali kuwasaka wauaji popote walipo.
Akitoa salamu katika ibada ya kumuaga marehemu Ndambo nyumbani kwake Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe Deo Sanga ameagiza kutafutwa kwa wahalifu na wauaji hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema jitihada za kuwatafuta waliohusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo zinaendelea huku akiwatoa hofu wananchi na kuwataka waendelee na Shughuli zao kama kawaida.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Njombe ambaye ni mkuu wa mkoa Antony Mtaka ameagiza kufanyika kwa Oparesheni maalumu itakayosaidia kubaini wahusika wa matukio ya mauaji yanayoendelea likiwemo la mfanyabiashara huyo wa miamala ya fedha.
Baadhi ya Wananchi na Wafanyabiashara mkoani Njombe akiwemo Alfred Nziku wameonesha kusikitishwa na matukio ya mauaji yanayofanyika huku wakiomba serikali kudhibiti vitendo hivyo.
Mauaji ya mfanyabiashara Godfrey Ndambo [45] yaliyofanyika nje ya geti la Nyumba yake majira ya usiku na kupora shilingi milioni 47 yamesababisha wafanyabiashara kufunga maduka yao kwa takribani saa 10 kwa lengo la kuikumbusha serikali kuimarisha ulinzi pamoja na kushiriki mazishi ya mwenzao.
0 Comments