Header Ads Widget

BILIONI 24 ZASOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI KWA MBUNGE MAKANIKA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

SHILINGI Bilioni 24 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma zinaelezwa kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi.

 

Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Asa Makanika alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Matyazo tarafa ya Kalinzi wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma akiwa kwenye ziara za kutembelea miradi mbalimbali na kuzungumza na wananchi katika jimbo hilo.

 

Makanika alisema kuwa katika fedha hizo zilizolewa na serikali ya awamu ya Sita ya Raisi Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu madarakani zimewezesha kujengwa kwa vituo vitatu vipya vya afya ambavyo tayari vimeanza kutoa huduma na kufanya jimbo hilo kuwa na vituo vitano vya afya kwa sasa

 

Sambamba na hilo Makanika alisema kuwa katika sekta ya afya wamekamilisha zahanati tano mpya katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma za afya kabisa na hivyo kuwezesha huduma kusogezwa karibu na wananchi.

 

Aidha alisema kuwa kwa kipindi hicho cha miaka mitatu fedha hizo zimeweza kutekeleza ujenzi wa shule 12 Mpya za sekondari ikiwemo shule maalum nne katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ikiwemo mwambao wa kaskazini wa ziwa Tanganyika ambako kuna miundo mbinu duni ya usafiri.

 

Mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kaskazini alisema kuwa Pamoja na fedha hizo zilizotolewa na serikali ambazo amekuwa na mchango mkubwa wa kupatikana kwake pia Mfuko wa jimbo umetumia kiasi cha shilingi milioni 57 katika kuchangia utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni tano kukamilisha darasa la shule ya msingi katika Kijiji cha Matyazo ambayo imekwama na wananchi kulazimika kuchangishwa ili kununua matofali 18,000 kumaliza darasa hilo hivyo mbunge ameamua kutoa fedha hizo ili wananchi wasiendelee kuchangishwa na kufanya mradi huo kukamilika.

 

Akiwa kwenye mkutano huo wa hadhara Makanika alipokea malalamiko ya wananchi wa Kijiji akiwemo Sophia Ndarichako ambaye amelalamikia wakandarasi wa TANESCO wanaoshughulika na utekelezaji wa umeme vijijini kupitisha nguzo katika shamba lake huku kukiwa hakuna maelezo yeyote kuhusiana na tukio hilo.

 

Kufuatia hali hiyo Mbunge Makanika amewataka wakandarasi wa TANESCO na REA kuwasilisha ramani za kazi zao kwa watendaji wa vijiji na kata ili kuona maeneo yanayopitisha miundo mbinu ya umeme badala ya kuamua njia ambazo haziko kwenye mpango na kusababisha migogoro na wananchi.

 

Makanika aliwaambia wananchi hao kuwa Pamoja na changamoto zinazojitokeza katika suala la kupeleka umeme kwenye vitongoji ameongea na viongozi wa TANESCO wanaosimamia mradi wa umeme vijijini ambapo wamekubaliana kuwa kuanzia Agosti Mosi mwaka huu upelekaji umeme kwenye vitoongoji vyote vya jimbo hilo utaanza.

 

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kigoma Vijijini, Halimesha Mayonga amewataka wananchi wa jimbo hilo wamuunge mkono mbunge huyo aweze kutekeleza majukumu yake katika kusimamia maendeleo kwa amani na utulivu.

 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI