Header Ads Widget

ABDUL NONDO AHIMIZA MABADILIKO YA MAENDELEO NCHINI



Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa Abdul Nondo amewataka wananchi kuacha uoga na kujionea wanyonge wakizoea tabu zinazowakabili akisema zimetengenezwa na mfumo mbovu wa Serikali kwa wananchi.


Nondo amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Stendi ya zamani Jimbo la Kondoa Mjini mkoani Dodoma kwenye ziara ya Kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu.


Kiongozi huyo wa vijana wa chama cha upinzani ACT Wazalendo, amesema Serikali ndio chanzo kikuu cha matatizo yanayowasibu wananchi kwani wananchi wengi wameendelea kuwa fukara huku maisha yakipanda bei.


Kutokana na mambo mbalimbali yanayowasibu wananchi, Mwenyekiti wa Ngome ya vijana nchini Tanzania Abdul Nondo, anawataka vijana na wananchi kwa ujumla kuacha uoga na unyonge badala yake wapambanie haki zao.


Amewataka kutumia uchaguzi ujao kuichagua ACT Wazalendo akidai Chama Cha Mapinduzi CCM kimeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na kwamba wananchi wana hali ngumu ya maisha na kughubikwa na lindi la ufukara ikiwemo wananchi wa Dodoma anaosema ni mkoa wa tano kwa umasikini nchini Tanzania.


Kiongozi huyo amewataka pia wananchi kuendelea kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo ili kuunganisha nguvu kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani.


Ikumbukwe haya yanajiri ikiwa ni kwenye mwendelezo wa ziara ya kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania Bi. Dorothy Semu anayoendelea nayo katika makao makuu ya Tanzania mkoani Dodoma ambapo pamoja na kuelimisha wananchi juu ya haki za uraia na maandalizi ya chaguzi pia ACT Wazalendo inasajili wanachama mpango uliozinduliwa Julai 22, 2024 katika jimbo la Mvumi Dodoma ambapo dhamira ya chama Cha ACT Wazalendo ni kusajili wanachama milion 10 kwa kipindi cha miezi 10.


Baada ya mikutano pamoja na maeneo ya majimbo ya Chemba na Bahi mkoani Dodoma, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Dorothy Semu ataendelea na mikutano ya hadhara katika majimbo na maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa awamu hii anafanya ziara katika mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, ziara ambayo itakwenda hadi Agosti 12, 2024.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI