Header Ads Widget

THRDC YATAKA UCHAGUZI MKUU UJAO UWE WA HURU NA HAKI.

Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetaka uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa uhuru na haki ili kuhakikisha kunakuwepo na uwakilishi wa kutosha wa wabunge kutoka kambi ya upinzani bungeni.

Wito huo umetolewa Dodoma na Wakili Onesmo Ole Ngurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, wakati wa mafunzo ya haki za binadamu yaliyoandaliwa kwa mawakili vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Ngurumwa amesema upungufu wa wabunge wa upinzani katika Bunge la 12 uliathiri uwezo wa Bunge katika kuisimamia Serikali, hali iliyopunguza hoja mbadala na kuongeza ukimya wa kimjadala ndani ya Bunge.

“Ushauri wangu ni kwamba uchaguzi mkuu ujao uwe wa huru na wa haki ili tupate Bunge lenye wabunge wengi wa upinzani. Tuwe na Bunge lenye nguvu ya hoja mbadala na siyo kimya kama lililopita,” alisema Ngurumwa.

Amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, bado kuna nafasi ya kufanya maboresho kupitia mchakato wa Katiba Mpya ili kuimarisha zaidi misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Ngurumwa alieleza kuwa wanasheria wana jukumu kubwa katika kulinda haki za wananchi kwa kuwa wanahusika moja kwa moja na uundaji wa sheria, usimamizi, tafsiri na utekelezaji wake.

Alieleza pia changamoto ya upungufu wa mawakili wanaotoa msaada wa kisheria, na kuwasihi mawakili vijana kupenda kujifunza, kujitolea na kushiriki kikamilifu katika kusaidia jamii zinazokosa uwezo wa kupata huduma hizo.

Kwa upande wake, Wakili Kasimu Semalani kutoka Mwanza, ambaye ni Kiongozi wa Kanda ya Ziwa wa THRDC, alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kushughulikia kesi mbalimbali zikiwemo za jinai, madai, biashara na masuala ya kijamii kwa kuzingatia haki za binadamu.

Amesema kazi ya uwakili haiwezi kutenganishwa na utetezi wa haki kwa kuwa karibu kila shauri linalohusika mahakamani linahusiana moja kwa moja na haki ya mtu binafsi au jamii.

Akizungumzia matukio ya watu kupotea, Semalani alisema THRDC tayari imetoa tamko la kulaani vitendo hivyo na kuunga mkono kauli ya Rais Samia inayolitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya wahusika wa utekaji na upoteaji wa watu.

“Kauli ya Rais ni thabiti, na sasa ni jukumu la vyombo vya dola kuhakikisha watu wote waliopotea wanapatikana na matukio hayo yanakomeshwa mara moja,” alisema.

Mafunzo hayo ya siku kadhaa yalitarajiwa kuwajengea mawakili vijana weledi na ari ya kujitolea katika kuendeleza misingi ya haki, usawa na utawala bora nchini.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI