Header Ads Widget

WANANCHI WAWASHTAKIA VIONGOZI WA KATA NA VIJIJI KWA MKUU WA WILAYA..

 


NA WILLIUM PAUL, SAME. 

BAADHI ya wakazi wa Kata ya Vumari wilayani Same wamewashtaki Viongozi wao kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni kuanzia ngazi ya Vitongoji hadi Kata kutoitisha mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kusoma mapata na matumizi hali ambayo imepelekea kuwepo kwa tuhuma za baadhi yao kupunguza kasi ya kujitolea katika shghuli za maendeleo.


Wakizungumza mbele ya Mkuu huyo wa wilaya kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kizungo wamesema zipo changamoto zinazowakabili ambazo zingeweza kutatuliwa ngazi ya Kata lakini hazitatuliwi wanasubiri mpaka viongozi wa wilaya wafike ndio wazitatue.


Aidha Mkuu wa Wilaya hiyo baada ya kuwasililiza wananchi amewaonya viongozi hao kuwa wakumbuke wamepewa dhamana ya kutatua kero na malalamiko ya wananchi wao na kwa wale watendaji wa serikali amewataka asiyetaka kazi ya kuwahudumia wananchi aache kazi kwani kuna vijana wengi wako hawana ajira na wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo.


Pia kwa Viongozi wa kuchaguliwa ambao Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji amewatahadharisha kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni hautahitaji kupata viongozi wazembe wasiotimiza wajibu wao na kuwataka wananchi kufanya uchaguzi sahihi mwaka huu ili wasijutie kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.


“Waoneeni huruma hawa wananchi wengine hapa ni wakuchaguliwa wengine tunalipwa mishahara ya Serikali lazima tutimize wajibu wetu Mtendaji wa Kijiji na Mtendaji wa Kata mnacheki namba nyie mnalipwa na Serikali, niwaombe sana wekeni ratiba za kusikiliza kero na mimi nipewe kopi kule ofisini kuanzia sasa mtaleta kwa Katibu Tawala wa wilaya nione kazi mnazofanya”. Alisema Kasilda.


Katika hatua nyingine Kasilda ametoa mwezi mmoja kwa Afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Same kufika Kitongoji cha Vumari Kata ya Vumari kutatua mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa takribani miaka kumi sasa, na akisha tatua atoe mrejesho wa namna alivyotatua.


Agizo hilo linakuja baada ya wakazi wa Kitongoji hicho kumweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa kuna wananchi wamevamia eneo la Kijiji kwa muda mrefu lakini Viongozi wa hapo hawajachukua hatua yeyote mpaka sasa.


Mwisho... 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI