Na Moses Ng'wat, Songwe.
MKUU mpya wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, ameapishwa rasmi kuanza majukumu yake mapya, huku akielezwa changamoto kadhaa anazopaswa kwenda kuzifanyia kazi, ikiwemo mimba za utotoni na magendo katika mpaka wa Tunduma.
Mwandobo ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ofisa mwandamizi, ofisi ya Rais Ikulu, hivi karibuni aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi ya Kenan Kihongosi ambaye kateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza baada ya kula kiapo, Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Momba amehidi kufanya kazi kwa nguvu zake zote na kusema yeye si mtu wa maneno mengi bali ni vitendo hivyo atakutana na watendaji kwenye maeneo ya kazi (field).
"Natoa shukrani za dhati kwa Rais kuniteua katika nafasi hii na uteuzi huu umeweka alama kubwa kwenye maisha yangu... na ninaahidi kufanya kazi kwa nguvu zangu zote na sitaki kuwa na maneno mengi tukukutane 'field' ". Alisisitiza Mwandobo.
Wakati Mkuu huyo wa Wilaya akieleza hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, akizungumza baada ya kukamilisha zoezi hilo la uapisho alitumia fursa hiyo kueleza changamoto kadhaa ambazo mkuu huyo wa Wilaya anapaswa kwenda kuzifanyia kazi.
Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni tatizo kubwa la mimba za utotoni, mdondoko wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, pamoja na vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Momba, Chobgolo alisema kuwa ndani ya mwezi mmoja wa Aprili pekee jumla ya watoto 194, wakiwemo wanafunzi katika Wilaya ya Momba walipewa mimba.
Kadhalika, Chongolo alimtaka Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha anasimamia vizuri mpaka wa tunduma ambao ni mpaka unaopitisha aslimia 75 bidhaa zinazo toka katika bandari ya Dar es salaam.
Alisema mpaka wa Tunduma ni lango kuu la nchi za kusini mwa Afrika hivyo ni vizuri udhibiti wa bidhaa ukafanyika ili serikali iweze kupata mapato na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.
Mwisho.
0 Comments