xxxxxxxxx
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TUME huru ya uchaguzi Tanzania (INEC) imetangaza kusogezwa mbele kwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililokuwa lianze Julai Mosi mkoani Kigoma na kwamba sasa zoezi hilo litaanza Julai 20 mwaka huu mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania, Jaji Jacobs Mwambegele ametoa tangazo hilo la tume mbele ya waandishi wa Habari mjini Kigoma jana akieleza kuwa kusogezwa mbele kwa zoezi hilo kunatokana na wadau wa uchaguzi waliotaka kupewa muda Zaidi kushiriki kutoa elimu na kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo la uboreshaji daftari.
Jaji Mwambegele alisema kuwa kabla ya kusogezwa mbele kwa zoezi hilo la uboreshaji daftari tayari tume imeshafanya mikutano tisa na wadau mbalimbali ambapo kati yao hiyo mikutano minane imefanyika Dar es Salaam na mkutano mmoja umefanyika mkoani Kigoma.
Alisema kuwa mikutano hiyo ilihusisha viongozi wa dini, wawakilishi wa asasi za kiraia, Wahariri wa vyombo vya Habari, waandishi wa Habari, maafisa Habari wa mikoa na Halmashauri, wawakilishi wa makundi maalum ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee wa kimila.
Pamoja na hilo alisema kuwa mipango ya uzinduzi ya zoezi hilo kufanyika mkoani Kigoma inaendelea kama awali na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Aidha mwenyekiti huyo wa Tume ameziomba asasi kuomba jukumu la kutoa elimu na uhamasishaji huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wadau wa uchaguzi kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa jamii lakini pia kuhamasisha wananchi waweze kujitokeza kwa wingi mchakato wa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura utakapoanza.
Akizungumzia kusogezwa mbele kwa muda wa kuanza kwa zoezi hilo Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Green shadow ya mjini Kigoma, Ignas kilongola ameipongeza tume kwa kuwa Sikivu kwa kuchukua hatua kulingana na maoni ya wadau katika kuboresha mchakato huo wa uboreshaji daftari.
Kilongola ambaye alikuwa mmoja wa wadau waliohudhuria mkutano wa tume hiyo na wadau wa uchaguzi wa mkoa Kigoma Juni 19 mwaka huu alisema kuwa wadau watatumia muda huo kuona namna wanavyoweza kufanikisha kusaidia zoezi hilo.
0 Comments