NA JOSEA SINKALA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Oran Manasse Njeza, amesema bajeti ya shilingi Billion 49 iliyopitishwa na Bunge la Tanzania kwa mwaka huu (2024/2025) inakwenda kujibu haja nyingi ambazo ni mahitaji ya wananchi.
Mhe. Njeza amesema hayo wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari jijini Dodoma kuhusu Bajeti kuu ya Serikali.
Amesema bajeti hiyo inakwenda kuwa majibu ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotarajiwa kwani imepanda kutoka Billion 44 hadi 49 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda kwa bidhaa.
Njeza amesema pia Kamati ya bajeti anayoiongoza ina kipengele cha bajeti ya dharula hivyo kunapokuwa na jambo la udharula na majanga kama kimbunga Hidaya, Serikali imejipanga kukabiliana nayo.
Alipoulizwa kuhusu kupanda kwa bajeti hiyo na maandalizi ya chaguzi za baadaye za kiserikali Mhe. Mwenyekiti huyo ambaye ndiye Mbunge wa Mbeya vijijini, amesema uchaguzi ni mpango uliopangwa (Planned event) hivyo bajeti yake haihusiani na bajeti kuu ya Serikali ambayo lengo lake ni kutumika kwa ajili ya Taifa kwa ujumla na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kuhusu maendeleo ya Jimbo lake la Mbeya vijijini ameishukuru Serikali kwa bajeti hiyo akiamini kuwa barabara nyingi zinakwenda kujengwa ili kuwa bora zaidi licha ya nyingine kuendelea kushughulikiwa.
Amezitaja baadhi ya barabara zilizo kwenye bajeti kuwa ni pamoja na ile ya Isyonje Makete, Mbalizi Shigamba na barabara ya Mbalizi Chang'ombe Mkwajuni hadi Makongolosi Wilayani Chunya na kuunganisha mikoa ya Tabora na Singida.
Aidha amesema ujenzi wa barabara ya njia nne katikati ya Jiji la Mbeya hadi jimboni kwake kutasaidia kupunguza ajali za mara kwa mara katika eneo la mlima Iwambi/Mteremko wa Mbalizi pamoja na mpango wa upanuzi wa barabara kuu kutoka Igawa Mbarali hadi Tunduma mkoani Songwe kutaboresha zaidi maisha ya wananchi.
0 Comments