Header Ads Widget

POLISI SONGWE INAWASAKA WATUHUMIWA WA WILAYANI MBOZI.

 


NA JOSEA SINKALA, SONGWE.


Polisi mkoani Songwe imesema kwa kushirikiana na wananchi inaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako na operesheni mbalimbali ambapo Polisi imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili kwa tuhuma za kuingiza bidhaa nchini bila kufuata utaratibu.


Pamoja na hayo Polisi inawatafuta watuhumiwa wa mauaji katika matukio mawili yaliyotokea wilayani Mbozi mnamo Juni 12, 2024 katika mji mdogo wa Mlowo Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.


Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe ACP Gallus Hyera, siku ya Juni 12,2024 Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa wawili  wote wanaume mmoja akiwa na umri wa miaka 51 dereva na mkazi wa Kimara Dar Es Salaam akiwa na mwenzake mwenye umri wa miaka 37 mfanyabiashara na mkazi wa Majengo Mjini Tunduma wilayani Momba wakiwa wanasafirisha Mapipa 136 ya Kemikali ya aina Ethano yenye ujazo wa lita 250 kila pipa ya kutengenezea pombe kali yakiwa kwenye gari aina ya Scania Horse namba T.231 ARN na Traller namba T.330 ECR ambalo lilikuwa linatoka Mji wa Tunduma likielekea Dar Es Salaam.


Taarifa hiyo ya Polisi, imeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mzigo huo ulikuwa umetokea Dar Es Salaam kwenda nchini Zambia kupitia mpaka wa Tunduma na kisha kurudishwa tena upande wa Tanzania kwa njia isiyo rasmi na kukwepa kodi ya Serikali ili kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.


Kaimu kamanda Hyera anasema kwa sasa upelelezi wa kina unaendelea ili kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusika katika tukio hilo ikiwa ni pamoja na mmiliki wa gari ili kuwafikisha Mahakamani.


Pamoja na tukio hilo, pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuwasaka watuhumiwa wa tuhuma za mauaji yaliyotokea katika kata ya Hasanga na Iyula Wilaya ya Mbozi Mkoani humo.


Tukio hilo lilitokea juni 13, 2024, huko maeneo ya Mpakani Kata ya Hasanga ambapo mwanaume mwenye umri kati ya miaka 22-25 ambaye hajatambulika alikutwa akiwa ameuawa kwa kuchomwa moto na mwili wake ukiwa na majeraha makubwa mawili moja likiwa kichwani na lingine mdomoni yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali na pembeni yake kulikuwa na kiroba chenye mahindi makavu.


Baada ya taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio hilo na kubaini kuwa tukio hilo lilianzia katika mtaa wa Ichenjezya shule ambapo mibuluzo na damu zilionekana mpaka sehemu ulipokutwa mwili wa marehemu.


Kutokana na mazingira ambayo mwili ulikutwa pakiwa na kiroba cha mahindi iliashiria kuwa marehemu alishambuliwa akituhumiwa kuiba mahindi hayo hata hivyo uchunguzi zaidi unafanyika ili kubaini sababu na chanzo cha mauaji hayo.


Pia mnamo Juni 14, 2024 katika kijiji cha Igale Kata ya Iyula Wilaya ya Mbozi mwanaume mmoja mwenye umri kati ya miaka 25-30 ambaye hajatambulika alikutwa akiwa ameuawa na mwili wake ukiwa na majereha sehemu mbalimbali na pembeni yake kulikuwa na fimbo na mawe.


Kamanda Hyera, uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo alikuwa na wenzake ambao walivunja kibanda cha biashara na kuiba pesa zilizokuwa ndani ya Bonanza baada ya kuvunja Bonanza hilo majira ya saa nane usiku, ndipo mlinzi wa eneo hilo alipopiga filimbi ili kupata msaada na wananchi walijitokeza na kufanikiwa kumkamata mmojawapo ambaye ameuawa baada ya kushambuliwa kwa fimbo na mawe maeneo ya kichwani na mwilini mpaka kumsababisha kifo chake.


Pamoja na kuzuia na kuepukana na uhalifu, pia Polisi Mkoani Songwe inaendelea kuitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kujeruhi au kuua wenzao badala ya kutumia njia sahihi kutatua matatizo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI