Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kupiga picha lori la mafuta lilioanguka.
Jackton amekamatwa muda mfupi uliopita na kupelekwa kituo kikuu cha polisi Same mjini hadi sasa.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Same ( DC) Kasilda Mgeni ameagiza Manyerere kuachiwa mara Moja.
Matukio Daima media inaendelea kumtafuta kamanda wa polisi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa taarifa zaidi .
TAARIFA YA MANYERERE
Ndugu zangu, Juni 15 polisi wilayani Same walikamata kwa ‘kosa’ la kupiga picha lori la mafuta ya kula lililopinduka. Kilikuwa kitendo cha uonevu na udhalilishaji. Nilinyang’anywa simu na vitu vingine.
Picha zikafutwa, lakini nikawambia ninao ujuzi wa kitaaluma wa kuzitunza kwa hiyo wasidhani zimepotea.
Niwahakikishie kuwa ninazo ingawa machoni waliona zimefutwa.
Nilifanikiwa, kwa kumtumia msamaria mwema, kupenyeza taarifa za kukamatwa kwangu.
Kilichotokea ni umma wa wana habari na jamii kujitokeza kwa wingi mno kulaani tukio hilo la uonevu na udhalilishaji.
Nimepokea simu nyingi mno. Nimetumiwa ujumbe mwingi-wa sauti, na wa maandishi.
Kwa hakika nimeuona upendo wenu. Sina la kusema zaidi ya kuwashukuru sana kwa wema na mshikamano mliouonyesha kwangu na kwa tasnia nzima ya habari. Mimi nimeachiwa kwa sababu ya sauti zetu, na pengine kwa kujulikana kwangu kidogo.
Je, wanyonge wangapi wanaoumizwa na mapolisi kwa kuwa tu hawana wa kuwasemea? Nawaomba tuendelee kuwa majasiri pindi tunapoonewa, au tunapoona binadamu wenzetu wakionewa.
Licha ya kwamba bado tunayo kazi kubwa kwenye safari ya kuifikia haki, usawa, na utu, naomba tusichoke. Asanteni sana sana sana.
Manyerere J.N
Juni 16, 2024
☎️karibu utangaze na Matukio Daima media piga 07447044508
0 Comments