Serikali imesema kuwa inatambua mahitaji na umuhimu wa kuanzisha maeneo ya kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Festo Dugange alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Mbeya Vijijini Mhe. Oran Njeza.
Katika swali lake Mbunge Njeza aliuliza ni lini Serikali itapandisha hadhi ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbalizi ndipo Naibu Waziri akatoa majibu ya Serikali.
Akijibu swali hilo ambalo ni kilio na ombi la muda mrefu la Mbunge wa Mbeya vijijini, Dugange amesema kuwa uanzishaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za wilaya) Sura 287 na (Mamlaka za miji) sura 288 pamoja na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala wa mwaka 2014.
"Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadae kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa ikiwemo mamlaka ya Mji mdogo wa Mbalizi", amesema Naibu Waziri Dugange.
0 Comments