Serikali wilayani Njombe imepiga marufuku wanunuzi wa parachichi kununua matunda hayo kwa kutumia maroba na badala yake watumie vipimo vilivyoelekezwa na wakala wa vipimo ambavyo ni creti huku changamoto ya bei ikitafutiwa muarobaini.
Aidha changamoto ya ununuaji parachichi kwa shilingi 200 kwa Kilo moja kwa kile kinachotajwa ni za daraja la pili yaani[Reject] pia imetajwa kusababisha wakulima kuanza kukata tamaa ya kilimo hicho kwani hali imekuwa mbaya hivi sasa inayohitaji serikali iingilie kati.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa wakati akizungumza na wakulima wa parachichi na Wanunuzi katika ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Njombe amesema hayuko tayari kuona wakulima wa Parachichi wanaingia kwenye mkwamo mkubwa wa soko la tunda hilo ilihali wakulima wametumia gharama kubwa katika uzalishaji.
Sanjari na hayo lakini pia Kasongwa amewaelekeza wanunuzi wote kuwatumia wataalamu wa Kilimo kuthibitisha kama Parachichi inayonunuliwa ni Daraja la pili yaani Reject vinginevyo itakuwa ni kuwaibia wakulima.
Baadhi ya wakulima wa Parachichi wilayani Njombe akiwemo Atukuzwe Mwendamseke,Essau Fute na Mchungaji Adamson Saki toka Kifanya wamesema hali imekuwa mbaya kutokana na kukosa njia mbadala ya kukabiliana na changamoto za maisha na ndio maana wanajikuta wanauza parachichi kwa bei ndogo.
Mkuu wa Idara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji wa Njombe Thadei Luoga anakiri kupokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.
Naye Ofisa Vipimo mkoa wa Njombe Shaban Kingu kwa Niaba ya meneja wa Vipimo anapiga marufu kutumia kipimo kingine tofauti na mzani kwenye zao la aina yoyote.
Kwa Upande wao baadhi ya wanunuzi wa Parachichi mkoani Njombe akiwemo Erasto Ngole licha ya kukiri kuhusika kwenye baadhi ya Changamoto lakini wamewataka wakulima kuzingatia ubora katika matunda yao kwani kimekuwa kikwazo katika soko la Kimataifa.
Parachichi katika mkoa wa Njombe limekuwa zao la Kimkakati ambalo lilionyesha kuwa na tija kubwa kwa wakulima jambo ambalo bei kwa sasa imekuwa kitendawili.
0 Comments