NA WILLIUM PAUL, SAME.
BAADA ya kupita Serikali tano za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hatimaye Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeandika historia mpya katika tarafa ya Mamba Vunta yenye jumla ya kata tano na vijiji 20 kwa kupeleka gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Afya Myamba.
Gari hilo limepokelewa kwa bashasha na cherekochereko kutoka kwa wananchi wapatao 47171 wa tarafa hiyo ambayo wanaishi katika milima ya Pare huku wakimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela.
Akikabidhi gari hilo kwa wananchi, Mbunge wa Jimbo hilo, Anne Kilango alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za Afya katika Jimbo hilo lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi.
Alisema kuwa, wakati Rais Samia anaingia madarakani jimbo hilo lilikuwa na kituo cha Afya kimoja cha Ndungu lakini katika kipindi chake cha miaka mitatu ameweza kuongeza vituo vya Afya viwili huku pia kwa sasa ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vingine pamoja na ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Jimbo la Same mashariki.
"Jimbo hili ili liendelee zaidi linahitaji Rais, Mbunge, Madiwani na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanaotokana na sisi ili waweze kushirikiana kwa pamoja hivyo wananchi msije kufanya makosa" Alisema Anne Kilango.
Na kuongeza " Jimbo hili ni gumu sio kila mtu anapenda kupanda milimani lakini mimi napenda kuja huku kwa sababu wananchi wa huku ni wachapakazi hivyo niwaombe tuungane kuhakikisha tunakuza maendeleo".
Mbunge huyo alisema kuwa, pia Jimbo hilo halijawahi kuwa na gari la kubebea wagonjwa ambapo wananchi walikuwa wakitumia gharama kubwa kuwasafirisha wagonjwa kwenda hospitali ya wilaya ya Same na mkoa lakini Serikali ya awamu ya sita imeweza kununua magari mawili ya kubebea wagonjwa katika kituo cha Afya Ndungu pamoja na kituo cha Afya Myamba.
Alisema kuwa, magari hayo ni ya kubebea wagonjwa na kuwataka madereva watakaokabidhiwa kuhakikisha wanayatumia kwa kazi iliyokusudiwa na sio kinyume na lengo.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo Mganga Mkuu wa wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander alisema kuwa, kituo hicho cha Afya Myamba kimegharimu milioni 757 ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu na mapato ya ndani ya halmashauri.
Alisema kuwa, kwa sasa kituo hicho kimeanza kutoa huduma ambapo kimeshawahudumia wagonjwa wa nje wapatao 1860, wamama wajawazito na watoto zaidi ya 300 wamepatiwa chanjo, na wajawazito 12 wamejifungua tangu kianze kutoa huduma mwezi Mei mwaka jana.
Aidha Mganga Mkuu huyo alisema kuwa, kujengwa kwa kituo hicho kimesaidia kupunguza adha kwa wananchi zaidi ya 40,000 ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali wa kilomita 36 kwa ajili ya kupata huduma za Afya.
Mwisho.
0 Comments