Na Fadhili Abdallah,Kigoma
VIONGOZI wa Chama Cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu (CHAKUHAWATA) wameongoza mamia ya walimu na wakazi wa mkoa wa Kigoma na mikoa mbalimbali ya Tanzania katika mazishi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Steven Sabibi (70) aliyezikwa kwenye kijiji cha kalinzi wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.
Sabibi ambaye alikuwa Mwanzilishi wa CHAKUWAHATA akiwa mwenyekiti wa chama hicho tangu kilipopata usajili mwaka 2015 hadi umauti ulipomkuta alifariki baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kutanuka moyo na shinikizo la damu, kiongozi huyo alifariki Jumanne wiki hii katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza katika misa ya mazishi ya Marehemu huyo yaliyofanyika katika kanisa Anglikana Kijiji cha Kalinzi, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Ashery Ntayomba alisema kuwa Marehemu Sabibi atakumbukwa kwa misimamo yake ya kupinga rushwa na kutetea haki za wafanyakazi zilizosababisha kuanzishwa kwa chama kipya cha CHAKUHAWATA kwa walimu waliojiengua na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).
Ntayomba alisema kuwa Marehemu ambaye mwaka 1984 alipata mafunzo ya Sanaa za maonyesho, michezo,muziki na elimu ya usimamizi wa uanzishaji wa vyama vya wafanyakazi katika nchi za Urusi, Jamhuri ya Check, Uswis na Slovania atakumbukwa kwa kazi kubwa ya kufundisha muziki na michezo aliyoanya kaztika shule mbalimbali mkoani Kigoma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHAKUHAWATA, Twalib Nyamkunga akizungumza katika misa ya mazishi alisema kuwa marehemu alitumia nguvu na juhudi zake kuhakikisha chama hicho kunakuwa na mafanikio hivyo kuwezesha CHAKUWAHATA kwa sasa kuwa na wanachama 31,000 mikoa yote ya Tanzania kutoka waanzishili 180 waliokuwepo mwaka 2015.
Steven Sabibi mmoja wa wanafamilia wa Marehemu Sabibi, akisoma wasifu wa marehemu alisema kuwa Mwenyekiti huyo aliajiriwa katika utumishi serikali mwaka 1977 baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu katika chuo cha ualimu Kabanga wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma mwaka 1976 hadi 1978 sambamba na kupitia mafunzo ya JKT kwenye kambi ya Bulombola mkoani Kigoma mwaka 1974.
Marehemu ambaye ameacha mjane na Watoto wanne alistaafu utumishi serikalini kwa hiari mwaka 2012 na kuanzisha harakati za kuundwa kwa Chama Cha kulinda na Kutetea haki za Walimu (CHAKUHAWATA) mwaka 1913 ambacho kilipata usajili mwaka 2015 na Marehemu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho tangu wakati huo hadi mauti yalipomkuta.
Mmoja wa wanafunzi wa marehemu Sabibi ambaye alifundishwa akiwa shule ya Msingi Muungano mjini Kigoma,Helena Jokala alisema kuwa anamkumbuka marehemu kwa mashairi, nyimbo na michezo mambo yaliyofanya wanafunzi wengi kupenda Kwenda shule kwa ajili ya kujifunza kutoka kwa mwalimu huyo.
Mwisho.
0 Comments