Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkoa wa Kigoma unaelezwa kupiga hatua katika kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama Kwenda kwa mtoto (PMTCT) huku mkakati ukiwekwa kuhakikisha mkoa huo unafanikisha kuzuia kabisa maambukizi hayo.
Meneja wa Mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) mkoani Kigoma, Dkt. Julius Zelothe alisema hayo katika ziara ya waandishi wa habari waliotembelea maeneo ambayo Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Dharula wa Raisi wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).
Dkt.Zelothe alisema kuwa tangu mwaka 2021 mradi wa Afya Hatua ulipoanza kufanya kazi zake mkoani Kigoma kwa kishirikiana na Serikali umeweza kupiga hatua katika kusaidia utoaji wa huduma za Kinga, Tiba na Matunzo, zikiwemo huduma za kudhibiti maambukizi ya Virus vya UKIMWI kutoka kwa mama Kwenda kwa mtoto ambapo kwa sasa hali ya maambukizi imepungua kutoka asilimia 1.3 mwaka 2022 na kufikia asilimia 1.0 kwa sasa.
Kwa upande wake Afisa ubakizaji na ufuatiliaji wa wapokea huduma, wa THPS Mkoa wa Kigoma, Juventus Julius alisema kuwa pamoja na mipango ya kudhibiti kabisa maambukizi ya VVU wanaendelea pia kuwahudumia wale wote ambao tayari wanaishi na maambukizi kwa kuwapatia huduma mbalimbali ikiwemo elimu na ushauri na kuwasimamia kuhakikisha wanapata dawa kwa wakati na wanazitumia vizuri.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu utekelezaji wa mradi wa Afya Hatua Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dkt. Isaya Mapunda alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza miradi ya Kudhibiti VVU na UKIMWI mkoani Kigoma ikiwemo THPS yamekuwa na mchango mkubwa kwenye kupunguza maambukizi na kuhudumia wapokea huduma.
Mapunda alisema kuwa kwa takwimu za sasa mkoa Kigoma una asilimia 1.7 ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI huku maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yakishuka kutoka asilimia 1.3 mwaka 2022 kufika asilimia 1.0 mwaka jana.
Akitoa ushuhuda kuhusu mafanikio hayo Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Rusimbi iliyopo katika Manispaa ya Kigoma, Dkt. Mathew Joram alisema kuwa tangu Oktoba mwaka jana hadi sasa Zahanati yake imewahudumia wanawake wajawazito 36 na kati yao 15 walijifungua huku mtoto mmoja tu akigundulika kuwa na maambukizi ambapo inaaminika yaliyotokana na mama kutofuata maelekezo ya daktali.
Naye Mama Kinara anayeishi na VVU na kutoa elimu kwa jamii, Bi. Golethe Ezekiel mwenye watoto watatu alisema kuwa alipata maambukizi tangu mwaka 2011 lakini katika muda huo hadi sasa amejifungua watoto wawili wote wakiwa hawana maambukizi.
Shirika la THPS kupitia Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua linahudumia vituo 69 vya Mkoa wa Kigoma kwa kutoa huduma mbalimbali za Kinga, Tiba na Matunzo.
Mwisho
0 Comments