Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kimewataka vijana wasomi wasikubali kutumika na kurubuniwa vibaya na watu wenye pesa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani 2025.
Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Singida, Elphas Lwanji, alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha viongozi wa matawi ya CCM ya vyuo na Vyuo Vikuu Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Singida.
"Kipindi hiki cha uchaguzi ndio kioindi cha kutumia fedha sana,msitumike vibaya na watu wenye fedha na mkawaambie wazee au wazazi eenu wasikubali kununuliwa wachague viongozi wazuri ambao watasaidia nchi kuleta maendeleo," alisema.
Lwanji alisema wasomi wanayo nafasi kubwa sana ya kutoa ushauri wale wanaoteua wagombea waweze kuwateua watu wazuri ambao wakichaguliwa watakuwa chachu ya kuleta maendeleo badala baadaye kusubiri kuja kulaumu kuchagua kiongozi asiyefaa.
"Tunaona kabisa huyu mbunge hatatufaa,huyu Mwenyekiti wa mtaa hatatufaa, huyu Mwenyekiti wa kijiji hatatufaa halafu mnanyanza kimya, hapana twendeni tukawashauri wazee wetu wachague viongozi sahihi na makini,"alisema.
Aidha,Lwanji aliwataka vijana kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wakazi ili wawe na nafasi nzuri ya kushiriki kupiga kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Alisema viongozi wa matawi katika vyuo ma vyuo vikuu wahakikishe wanahamasisha watu waweze kujiunga katika chama sanjari na kulipa ada ya uachama.
"Ili uweze kusajiriwa kidigitali ni lazima uwe na kadi ya CCM na ili uwe mwanachama hai lazima ulipie kadi ya uanachama maana huwezi kuwa kiongozi kama huna wanachama wengi kwenye eneo lako," alisema.
Lwanji aliwataka wasomi hao kutumia mitandao vizuri kwa ajili ya kujifunzia lakini wasiitumie kwa mambo mabaya kwani nchi inawategemea kuja kuwa viongozi wazuri wa baadaye.
MWENYEKITI UVCCM SINGIDA: CCM INAWATEGEMEA SANA VIJANA WASOMI
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Singida Mjini, Mohamed Msaghaa, alisema wasomi ndio kundi ambalo linapima na kuchakata mambo hivyo wanategemewa sana katika chaguzi za mwaka huu na mwakani kwani uwepo wao ndani ya CCM watakuwa viongozi bora.
Alisema ili wasomi waweze kupata nafasi ya kushiriki kupiga kura na kuwachaguzi viongozi wazuri wahakikishe wanajiandikisha kwani uchaguzi wa mwaka huu hautegemei kitambulisho cha mpiga kura.
"Mwaka 2025 nafasi ya urais tuna mgombea wetu ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo makubwa, ameongeza bumu amejenga shule,ametoa ajira na inaendelea kutolewa, mikopo ya asilimia 10 itaanza kutolewa Julai, kwa hiyo sisi kama vijana hatuna budi kumuunga mkono," alisema.
SENET UVCCM MKOA SINGIDA YATOA ONYO KWA TUNDU LISSU
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Senet Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida,Masatu Salum,alitoa onyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa,Tundu Lissu kuacha tabia ya kuzungumza mambo ukabila,udini na Muungano ambayo yanachochea vurugu nchini.
Alisema Lissu anapaswa kutambua kuwa rais Samia Suluhu Hassan ametoa uhuru kwa vyama kufanya siasa nchini lakini uhuru huo usitumike vibaya kwa kuzungumza mambo ambayo yatavuruga amani nchini.
Salum alisema kauli ya Lissu kwamba pikipiki walizogawiwa viongozi wa CCM eti zimenunuliwa na serikali ni kauli mfu ambayo haina ukweli kwasababu chama kila miradi mingi inayokiingizia fedha hivyo hakishindwi kununua pikipiki kwa fedha zake.
"CCM ina wanachama zaidi ya milioni sita hivyo wanapolipa ada ya uanachama ukijumlisha na miradi ya chama zinapatikana fedha nyingi ambazo zinatosheleza kununua pikipiki za chama," alisema Salum.
Alisema inashanga Lissu anazuia wananchi wasichangie katika shughuli za maendeleo lakini wakati huo huo yeye anatembeza bakuri kutaka wananchi wamchangie anunue gari jipya la kutembelea.
Salum aliongeza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu wasomi wa Mkoa wa Singida wanamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa asilimia 100 kwasababu ni mlezi wa wana.
Naye Mlezi wa Seneti Mkoa wa Singida, Salum Kanyungu,alisema wanavyuo ambao ni wanachama wa CCM ni muhimu sana kuzingatia maadili na nidhamu kwani taifa linawategemea sana kuja kuwa viongozi bora.
"Mjiepushe na matumizi mabaya ya simu kwa kujirekodi na kutuma kwenye mitandao ya kijamii mambo ambayo hayana maadili, pia kwenye vikao mjitahidi muwe mnavaa sare za chama," alisema.
MWISHO
0 Comments