Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kutekelezwa kwa mpango wa kliniki tembezi maarufu kama mkoba ya huduma za kinga, tiba na matunzo (CTC) kupitia shirika la THPS imewezesha kufikiwa kwa idadi kubwa ya wapokea huduma wanaoishi na maambukizi ya VVU wanaoishi katika maeneo ya pembezoni kwa kuwawezesha kupata dawa na kuzitumia kwa wakati.
Meneja Mradi wa Afya Hatua Wilaya ya Uvinza Dkt. Gabriel Max wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani humo iliyolenga kuangalia utekelezaji wa mradi wa afya hatua unaotekelezwa na shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na ukimwi (PEPFAR) kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha marekani (U.S. CDC).
Dk.Max alisema kuwa huduma ya mkoba imesaidia wapokea huduma kufika kwenye maeneo yaliyotengwa kwa wakati kupata huduma, kupata dawa kwa wakati na sasa wanafuata ratiba kikamilifu kwa siku za kupata dawa hivyo kufubaza VVU na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo baada ya afya zao kuimarika.
Meneja huyo alisema kuwa kwa sasa mpango huo unahudumia vituo 16 katika wilaya Uvinza zikihusisha huduma za tiba na matunzo, Upimaji, Uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama wanaoishi na VVU kwenda kwa mtoto na Tohara Kinga kukiwa na jumla ya wapokea huduma 6000 na kati yao watu 2000 wanafikiwa kwa njia ya mkoba.
Akizungumza katika ziara hiyo Muuguzi kutoka kituo cha Afya Uvinza, Dkt. Said Hamis Said amesema Kituo cha afya Uvinza kinahudumia wateja 780 ambao wana maambukizi ya VVU na sehemu ambayo wanapokea wateja wengi ni kutoka kwenye vituo vya Huduma MKOBA ikiwemo Tandala ambako hakuna kituo chochote cha kutoa huduma za afya na hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji cha Tandala kwenye Kijiji cha Chakuru wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Ngasa Kamishe alisema kuwa kuwepo kwa huduma ya mkoba kwenye kitongoji hicho imesaidia walengwa kupata huduma kwa urahisi, kwa wakati lakini pia kupunguza gharama kutembelea umbali wa kilometa 50 kufuata huduma kituo cha afya Uvinza.
Mmoja wa Wapokea Huduma kutoka kitongoji cha Tandala Kijiji cha Chakuru wilaya ya Uvinza, Joshua Zengo aliyebainika kuwa na maambukizi ya VVU mwaka 2018 anasema awali walikuwa wanapata huduma za tiba na matunzo katika kituo cha Afya Uvinza ambacho kipo mbali sana na eneo hilo hali iliyokuwa inapelekea baadhi kushindwa Kwenda kupata huduma hizo na hivyo kutofuata taratibu za kutumia dawa na wengi kukabiliwa na magonjwa nyemelezi.
Hata hivyo mpokea huduma huyo anaeleza kuwa uwepo wa Kliniki hiyo ya Mkoba imekuwa na faida kubwa kwao kwani imewapunguzia gharama na muda wa kufuata huduma kwenye kituo cha Afya Uvinza na hivyo kuwa wafuasi na watumiaji wazuri wa dawa za kufubaza VVU (ARV) na wengi wao kwa sasa afya zimeimarika.
Mwisho.
0 Comments