NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo BAZECHA mkoa wa Mbeya John David Mwambingija amesema alipogombea ubunge katika jimbo la Rungwe mwaka 2015 alishinda isipokuwa Chama cha Mapinduzi kiligeuza matokeo na kumpa ushindi mgombea wake wa ubunge wa wakati huo Sauli Amon.
Mwambigija amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika tawi la Ilundo kata ya Kiwira Wilayani Rungwe huko katika mkoa wa Mbeya.
Amesema wakati amegombea ubunge mwaka 2015 katika jimbo hilo wanachama wa vyama vyote na wasimamizi wa kura walimchagua hivyo kutokana na kuminywa kwa mikutano ya hadhara kwa miaka kadhaa alishindwa kuwashukuru hivyo kutumia mkutano huo kuwashukuru wote kwa kumchagua licha ya kutotangazwa na kuwaasa kujiandaa na chaguzi zijazo kuhakikisha CHADEMA inashinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, amewataka wananchi katika kata ya Kiwira na Wilaya ya Rungwe kwa ujumla kuachana na Chama Cha Mapinduzi na kujiuunga na CHADEMA kwa madai kuwa CCM ndio chanzo cha mateso yao.
Pamoja na huyo, Mwambigija aliambatana na viongozi wengine wa CHADEMA akiwemo Joyce Mwalalika ambaye ni mweka hazina wa Baraza la wanawake wa chama hicho na Saada Atiki ambaye alikuwa Diwani kata ya Manga jijini Mbeya ambao wamewashauri wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chaguzi zijazo wakisema wanawake ni chimbuko la maendeleo.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama tisa waliokuwa Chama Cha Mapinduzi CCM wamerudisha kadi za CCM na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kupokelewa na Mwenyekiti huyo wa Baraza la wazee wa CHADEMA mkoa wa Mbeya.
0 Comments