NA WILLIUM PAUL, SAME.
JESHI la Polisi mkoa wa Kilimanjaro lililazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya Wananchi zaidi ya mia sita (600) waliokuwa wamevamia lori lilokuwa limebeba mafuta ya kula aina ya korie lililopata ajali eneo la Njoro wilaya ya Same.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa alisema kuwa tukio hilo limetokea Juni 14 mwaka huu ambapo gari lenye namba za usajili T783 CTC aina ya HOWO na trela yake namba T.889 CSK likitokea Dar es salaam kuelekea Arusha liliacha barabara na kupinduka na kusababisha uharibifu wa gari hilo.
Alisema kuwa baada ya ajali hiyo kutokea taarifa zilifika kituo cha Polisi na askari waliwahi katika eneo hilo ambapo waliwakuta Wananchi wamevamia gari hilo kwa lengo la kupora mafuta hayo pamoja na jitihada zingine zilizochukuliwa kuwazuia wasiendelee kupora ililazimika Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya katika eneo hilo.
Aidha, askari mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu (jiwe) kichwani na mwananchi aliyekuwa akipinga amri ya kutawanyika eneo hilo.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro limetoa wito kwa Wananchi kuacha tabia ya kukimbilia kwenye eneo ambalo ajali imetokea kwa lengo la kufanya uporaji.
Aidha, wanapozuiwa na Askari kuingia kwenye eneo la tukio wawe wasikivu kwa usalama wao na watambue wakikaidi lazima hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kukamatwa.
Mwisho..
0 Comments