Header Ads Widget

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WAHIMIZWA KUHAMASISHA WANANCHI NA WADAU KUTOA MAONI DIRA YA MAENDELEO 2050

 




NA THABIT MADAI, ZANZIBAR 



WAKUU wa Mikoa na Wilaya Nchini wametakiwa kuhakikisha wanahamasisha Wananchi na wadau mbalimbali katika kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 ili kusaidia timu ya kukusanya maoni kupata maoni ambayo yatakayoakisi mahitaji halisi yanayoendana na wakati.




Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohammed wakati akofungua Semina ya Siku moja ya wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhusu uelimishaji wa umma na utaratibu wa zoezi la ukusanyaji maoni ya maendeleo ya 2050.




Amesema kuwa, ni wajibu wa Wakuu wa mikoa na Wilaya kuhakikisha zoezi la ukusanyaji wa maoni linafanyika kama ilivyokisudiwa kwa Amani na utulivu.




Pia amesema kuwa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanawajibu wa kusimamia na kuhakikisha zoezi la uhamasishaji wananchi kushiriki kutoa maoni linafanyika katika halmashauri za mikoa husika.




"Kushirikia mahojiano maalum na kutoa maoni kuhusu maandalizi ya Dira ya taifa ya maendeleo 2050," ameeleza.



Aidha amesisitiza kuwa wanawajibu wa kutoa kipaumbele cha pekee katika ushirikishwaji wa Makundi yote ya Wananchi pamoja na kutoa ushirikiano kwa timu za Wataalamu.



"Munatakiwa kutoa ushirikiano kwa timu za Wataalamu zitakazotembelea mikoa na wilaya kwa ajili ya ukusanyaji wa maoni kwa wananchi kwa njia ya mahojiano," amesema.



"Hata hivyo munatakiwa kuandaa vikao na watendaji katika ngazi zote za utawala ili kuwapa elimu ya Dira ya taifa ya maendeleo na umuhimu wake," ameeleza.





Mapema Mwenyekiti wa Timu kuu ya Wataalam ya Maandalizi ya Dira ya Maendeleo 2050 Prof. Lucian Msambichaka amesema kwamba, Semina hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa ufikiwaji wa wananchi katika zoezi la ukusanyaji wa maoni.




"Tunaomba tupate ushirikiano kutoka sehemu mbalimbali hivyo tunameona kuna haja ya kuwapa Semina Wakuu wa Wilaya na mikoa ili zoezi la ukusanyaji wa maoni liweze kufanikiwa kwa urahisi," ameeleza.




Nae Mkuu wa Wilaya ya Kaskazin A Othman Maulid ameshukuru timu ya Wataalam kwa kuandaa Semina hiyo na kuwaomba Wananchi na Taasisi mbalimbali kutoa ushirikiani kwa timu hiyo ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.




Mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ulizinduliwa Disemba 09, 2023 na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Dodoma.



000

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI