NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Afisa elimu msingi na awali wa Halmashauri ya Mbeya Mwalimu Tanu Kameka, amewapongeza walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Kata ya Shizuvi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutiwa moyo kwenye utendaji wao wa kazi ili kuongeza ari ya ufundishaji na kuongeza ufaulu wa watoto shuleni shuleni.
Mwalimu Kameka, amesema hayo akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Paul Sweya kwenye hafla ya kuwapongeza walimu kwa kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne.
Hafla hiyo imefanyika katika shule ya Sekondari Shisyete kata ya Shizuvi ambayo imeandaliwa na diwani wa Kata ya Shizuvi Mhe. Noah Mwashibanda ili kuwapa motisha walimu hao na kusaidia kuongeza bidii ya kufundisha ili kuendelea kuinua ufaulu katika shule zote za kata hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Diwani Mwashibanda amesema lengo lake ni kuona kata yao inatoka hatua moja kwenda nyingine ya juu zaidi kielimu kwani suala la elimu limekuwa likipuuzwa na baadhi ya wananchi hata kuwafanya kutozingatia kuwasomesha watoto wao.
Mhe. Mwashibanda, ametoa mitungi ya nishati ya kupikia (Gas) kwa ajili ya walimu wakuu kutumia shuleni hapo katika Kata yake.
Mgeni rasmi huyo Tanu Kameka amewaasa walimu kuendelea kufanya kazi kwa weledi, juhudi na maarifa ili kuongeza ufaulu katika shule zote za kata hiyo na jimbo la Mbeya vijijini kwa ujumla.
Kata ya Shizuvi Wilayani Mbeya ni miongoni mwa Kata 28 za Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambayo ilikuwa ikifanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya Taifa kuanzia shule za msingi hadi Sekondari na changamoto nyinginezo ikiwemo watoto kukatisha masomo na kwenda kuolewa au kufanya shughuli mbalimbali hivyo Kata hiyo kuazimia kuanza ujenzi wa mabweni, kusisitiza upatikanaji wa chakula shuleni na sasa motisha hiyo kwa watumishi mambo ambayo yatasaidia kuzingatia elimu na kuwakomboa watoto kielimu.
0 Comments