![]() |
Mkuu wa wilaya kigoma Salum Kali akizindua kambi ya matibabu ya madaktari bingwa kwa niaba ya mkuu wa mkoa Kigoma |
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MAMIA ya wananchi wa mkoa Kigoma wamejitokeza kwa ajiili ya kupata huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa 60 ambapo watapiga kambi ya siku tano kutoka huduma kwa wananchi wa mkoa Kigoma na mikoa Jirani.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa Kigoma Maweni, Stanley Binagi akizungumza na waandishi wa Habari hospitalini hapo alisema kuwa hadi kufikia mchana katika siku ya kwanza ya kambi hiyo watu 800 walikuwa wamejiandikisha ili kuanza matibabu.
Binagi alisema kuwa katika siku tano za kambi hiyo wanatarajia kuwafikia watu 3000 na kwamba hayo ni makadirio lakini idadi yeyote ya watu itakayojitokeza katika muda huo itahudumiwa na hakuna mtu aliyesajiliwa atakosa huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa Pamoja na wananchi wa mkoa Kigoma na mikoa Jirani pia wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Burundi wanatarajia kufaidika na huduma ya kambi hiyo ya madaktari bingwa iliyoanza mkoani Kigoma.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa kambi hiyo ya madaktari bingwa ni sehemu ya mpango wa serikali kusogeza huduma karibu na wananchi katika mpango wa Raisi Samia Suluhu Hassan kuboresha utoaji huduma kwenye sekta ya afya nchini.
![]() |
Mamia ya wananchi wa mkoa Kigoma waliojitokeza kwenye kambi ya madaktari bingwa katika mkoa Kigoma Maweni ambapo madaktari 60 wanatarajia kutoa huduma kwenye kambi hiyo |
Kambi hiyo ya matibabu inatarajia kuhudumiwa na madaktari bingwa kutoka mikoa ya Tabora,Rukwa,Katavi na wenyeji Kigoma sambamba na madaktari kutoka Hospitali za Bugando Mwanza, KCMC ya Kilimanjaro, Muhimbili Dar es Salaam na Benjamen Mkapa ya Dodoma ambapo magonjwa 15 yatashughulikiwa
0 Comments