Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida limewakamata watu 235 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai yakiwemo ya ubakaji na ulawiti katika doria na misako ya kutanzua na kuzuia uharifu iliyofanyika mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, SACP Amon Kakwale,akizungumza na waandishi wa habari leo (Aprili 6, 2024) amesema watu hao wamekamatwa katika kipindi cha kuanzia Februari hadi Aprili mwak huu katika misako mbalimbali iliyofanyika.
Amesema kati hao, watuhumiwa 135 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina Bhangi zenye uzito wa kilo 17 2, watuhumiwa 46 walikamatwa na Mirungi kilo 92, watuhumiwa wengine watano walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Heroini zenye uzito wa grams 0.82.
Kamanda Kakwale amesema watuhumiwa wengine 11 walikamatwa wakiwa na pombe ya moshi (gongo) lita 123, watatu wakiwa na ndoo 31 za mafuta ya kupikia aina ya safi mali ya kampuni ya Mohamed Enterprises Limited zenye ujazo wa lita 20 kila moja.
Watuhumiwa wengine watano walikamatwa na televisheni 'flat screen' 6 aina ya Hisense inchi 43,Samsung inchi 65,Samsung inchi 40 na TV nyingine mbili zikiwa zimefutwa majina ambazo ni mali za wizi.
Kamanda Kakwale ameongeza kuwa katika misako na doria hizo walikamata watuhumiwa watatu wanaojihusisha na hujuma katika miundombinu ya umeme wakiwa na transformation 159KVA namba TX006524 aina ya TCO yenye thamani ya Sh.milioni 7.5 pamoja na nyaya za shaba.
Ameongeza kuwa watuhumiwa wengine watatu walikamatwa wakiwa na miundombinu ya umeme ya Shirika la Ugavi Umeme (TANESCO) vipande 63 vya Polymeric Post Insulators ambavyo walivifunga kwenye viroba nane tayari kwa ajiri ya kuvisafirisha kwenda kuviuza mkoani Singida.
Kamanda Kakwale amesema watuhumiwa wengine wawili walikamatwa wakiwa na betri 7 za minara ya simu aina ya North Star zenye uwezo wa N-170 mali ya kampuni ya Helois Tower Tanzania na wengine wanne walikamatwa kwa kosa la kukutwa ba jenereta aina ya Parking Portableenye uzito wa tani moja mali ya kampuni ya minara ya simu ya Noven.
Aidha,watuhumiwa 11 walikamatwa kwa makosa ya wizi wa pikipiki (bodaboda), wanne kwa wizi wa pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji).
"Baada ya ukamataji huo,baadhi ya kesi zipo chini ya upelelezi,zingine zimefikishqa mahakamani zikiendelea kusikilizwa na zipo zilizopata mafanikio kwa watuhumiwa kuhukumiwa vifungo mbalimbali," amesema.
Amesema baadhi ya mafanikio ya kesi zilizofikishws mahakamani kwa kipindi hicho ni pamoja na Mustafa Hamis (35) kuhukumiwa kifungo cha maisha maisha jela kwa kosa la kulawiti na kubaka, Musa Masanilo (35) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka na Baraka Yohana (23) amehukumiwa jela miaka 39 kwa kosa la kubaka.
Kamanda Kakwale amesema Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama barabarani limefanya doria na misako na kufanikiwa kuwakamata madereva wawili kwa makosa muendesha magari jwa mwendo kasi usioruhusiwa kisheria.
Aliwataja madereva waliokamatwa kuwa ni Athuman Kasenya (34) ambaye ni dereva wa basi lenye namba za usajiri T 454 DHP mali ya kampuni ya Matunduru na Julius Dionice (39) dereva wa basi la kampuni ya Satco lenye namba T 937 EFK.
"Kutokana na makosa hayo,madereva hao walifungiwa leseni zao za udereva kwa kipindi cha miezi mitatu kwa uendeshaji wa gari kwa njia ya hatari na isiyofaa jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wengine wa barabara," amesema.
Kamanda Kakwale amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu ili wakamatwe mapema kabla hawajaleta madhara kwa jamii na waliopotelewa na na vitu vyao wafike kwenye vituo vya polisi wakiwa na risiti halisi za manunuzi ya vitu hivyo ili waweze kutambua na kukabidhiwa mali zao.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawashukru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kufanikisha ukamataji wa watuhumiwa hao 235 na vielelezo," amesema Kamanda Kakwale.
0 Comments