Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (mstaafu), Hayati Cleopa David Msuya, umefikishwa katika Viwanja vya Cleopa David Msuya, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro leo Mei 12, 2025 kwa ajili ya kuagwa rasmi na wananchi wa mkoa huo.
Mwili huo uliwasili majira ya saa nne asubuhi ukisindikizwa na msafara wa viongozi mbalimbali wa serikali, maafisa wa jeshi, pamoja na wajumbe wa familia. Shughuli hizo zilifanyika kwa utaratibu maalum uliopangwa na serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
Mamia ya wakazi wa Mwanga na maeneo ya jirani walijitokeza mapema kushuhudia tukio hilo la kihistoria huku wengine wakibeba mabango yaliyosomeka “Asante Mzee Msuya kwa utumishi wako wa mfano.” Wananchi walieleza masikitiko yao kutokana na msiba huo mkubwa lakini pia walielezea fahari kwa maisha ya uadilifu aliyoyaishi.
Viongozi wengine waliotoa salamu zao walimtaja Hayati Msuya kama kiongozi mwenye hekima, mnyenyekevu, na mwenye kujali maslahi ya watu. Walisema taifa limepoteza hazina kubwa, lakini mafundisho na maadili aliyoyaacha yataendelea kuwa dira kwa viongozi wa sasa na vizazi vijavyo.
Mazishi ya hayati msuya yanataraji kufanyika kijijini kwake Kirimeni wilayani Mwanga Mei 13, 2025.ambapo vionngozi Mbalimbali na Wananchi wataungana kumpa Heshima za mwisho
0 Comments