Header Ads Widget

DC KASILDA MGENI ACHARUKA UJENZI WA MAJENGO YA KITUO CHA AFYA MTII KUWA CHINI YA KIWANGO.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME


MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kumchukulia hatua Mhandisi aliyesimamia ujenzi wa kituo cha afya  kata ya Mtii wilayani humo kwa uzembe kushindwa kusimamia kikamilifu mradi huo na kusababisha baadhi ya Majengo kuwa chini ya kiwango.
 

Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake alipotembelea kituo hicho na kubaini moja ya majengo ya kituo hicho kuwa na nyufa hali ambayo inatishia usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaopata huduma kwenye kituo hicho ambacho tayari kimeanza kutoa huduma  kwa baadhi ya majengo yake  yaliyojengwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hicho.
 

Mbali na agizo hilo kutaka Mhandisi aliyesimamia ujenzi kuchukuliwa hatua Mkuu huyo wa wilaya ameagiza pia kumkamata mkandarasi aliyetekeleza mradi huo kwa uzembe wa kujenga mradi chini ya kiwango.
 


“Siwezi kukukabali uzembe wa aina hii nimekuja hapa kwa zaidi ya mara tatu na mara zote  kila nikija simkuti Mhandisi wa Halmashauri anawaacha mafundi  peke yao, na huyu mkandarasi aliyekuwa akijenga hapa  pia akamatwe popote  alipo kwa uzembe  huu  kama msimamizi mkuu wa miradi kwenye Wilaya ya Same  sitakubali  hujuma ya aina hii kuendelea”. Alisema Kasilda.
 


Na kuongeza "hata kwenye miradi mingine ambayo nimekua nikitembelea nimebaini Mhandisi huwa anakuja siku moja kabla ya ziara zangu na hii inaathiri kasi ya utendaji miradi mingi kuchelewa kukamilika kwakua hakuna ufuatiliaji wa karibu kwa wataalam ambao wanalipwa fedha na serikali kwa ajili ya kazi hiyo”.
 

Mradi huo wa ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mtii umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 500 fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kulenga kuboresha huduma ambapo kwa mujibu wa mkuu wa wilaya kwenye ufuatiliaji amebaini Mhandisi wa Halmashauri amekuwa na tabia ya kuwaacha mafundi pekee bila usimamizi hali ambayo ndio imesababisha majengo kuwa chini ya kiwango.
 


Baada ya kukagua mradi huo amefanya mkutano na wananchi wa kata hiyo na kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi lakini pia kuwasisitiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kutumia haki yao kuchagua na kuchaguliwa.

Mwisho.. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS