Peter Simon Msigwa,
M/kiti Kanda ya Nyasa,
Iringa.
Katibu Mkuu,
Chama cha Demokrasia na Maendeleo,
Dar es Salaam.
Yah: Malalamiko Dhidi ya John Mrema - Mjumbe wa Sekretariat*
Mheshimiwa Katibu Mkuu,
Nakuandikia kufikisha malalamiko yangu rasmi juu ya John Mrema Mjumbe wa Sekretariat.
Mwenendo wa John Mrema unazua maswali na anaonyesha ana maslahi dhidi ya uchaguzi wa Nyasa kwa kuonyesha dhahiri kuwa ana upande wa Mgombea ndugu Joseph Mbilinyi.
Kwasababu hiyo ninaamini hawezi kutenda haki hata kidogo katika uchaguzi huu ikiwa atashiriki kwa namna yoyote ile.
Kwa mantiki hiyo nayaleta malalamiko rasmi kwako kwa hatua zaidi za dharula kwa lengo la kulinda Demokrasia, kama tunavyohubiri mara zote.
1. Siku ya tarehe 24.05.2024 kabla na baada ya uchaguzi wa chama wa Mkoa wa Iringa, kuanzia majira ya asubuhi lakini pia saa kumi na mbili jioni alikutana na Mgombea Mwenzangu wa Kanda Nyasa katika nafasi ya Uenyekiti Mhe. Joseph Mbilinyi Twiga Night Club, ambapo Mgombea Mwenzangu aliweza kununua Cret 4 za Bia wakaendelea kunywa na Msimamizi huyu wa uchaguzi mpaka majira ya saa sita usiku.
i. Matukio haya yalifanyika mbele ya wanachama wafuatao ambao waliyashuhudia kwa kuona bila kusimuliwa, Mimi Mwenyewe Peter Simon Msigwa na wanachama wengine.
ii. Tarehe 26.05.2024 Mhe. John Mrema Msimamizi wa Uchaguzi walipanda gari ya Mgombea Uenyekiti wa BAVICHA Kanda ya Nyasa Mh.Vitusi Nkuna Kutoka Iringa Mpaka m
Makambako huku akijua kabisa mgombea uenyekiti wa Bavicha katika Kanda hii siyo huyo peke yake na ifahamike hata siku ya tarehe 24.05.2024 ndiye aliyekuwa anakunywa nae pombe mpaka usiku wa manane.
Kwa mazingira haya na kwa mantiki hiyo naamini kwamba Bw.John Mrema hawezi kutenda haki katika uchaguzi huu.
iii. Kwamba, kwa nyakati tofauti tofauti amekuwa akiwapigia simu wajumbe/wapiga kura katika ngazi ya Kanda akiwashawishi kwamba wasinichague mimi Peter Simon Msigwa bali wamchague Mhe. Joseph Mbilinyi kwani mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mheshimiwa Freeman Mbowe ameagiza Joseph Mbilinyi awe mwenyekiti na mimi sihitajiki na Mwenyekiti kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa.
Walioshawishiwa hivyo ni wajumbe wengi tukianza na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Iringa ambaye pia ameagizwa amchague Vitus Nkuna kwani ndiye viongozi wa kitaifa wanaye mtaka jambo ambalo ni kinyume na Kanuni ya 1 (vi) ya Mwongozo wa Chama dhidi ya Rushwa Kwenye Uchaguzi ndani ya Chama Toleo la 2012.
Vilevile Msimamizi John Mrema alimuita M/Kiti wa BAVICHA Mkoa wa Mbeya na kumuelekeza kwamba ampigie kura Joseph Mbilinyi na asipige kura kwa Msigwa, kwa madai kwamba Msigwa hahitajiki na Makao makuu.
Kwamba ni ukweli usiopingika kuwa John Mrema ameonyesha maslahi binafsi na baadhi ya wagombea hasa Joseph Mbilinyi na Vitus Nkuna, hivyo ni dhahiri kwamba ana mgongano wa kimaslahi kiasi kwamba hatotenda haki katika kusimamia uchaguzi kwani ana watu wake ambao anataka washinde uchaguzi huu huku akiwapigia kampeni kinyume na kanuni na taratibu za Uchaguzi. Lakini pia ni kinyume na Kanuni ya 10 (viii) na (ix) ya maadili ya Viongozi yanayokataza aina yoyote ya rushwa na kujihusisha na makundi ambayo mwisho wa siku itasababisha vurugu/mpasuko ndani ya chama kwa kiongozi.
Kutokana na hali hii, naomba yafuatayo yaweze kufanyika kwa udharula ili kukinusuru chama kisijekuingia kwenye migogoro katika Kanda ya Nyasa bila sababu za msingi;
1. Kuondolewa na kutojihusisha na shughuli zinazohusiana na usimamizi wa uchaguzi.
2. Waletwe wasimamizi wengine ambao hawana maslahi binafsi katika uchaguzi huu ili haki iweze kutendeka kwa wagombea wote bila ubaguzi wala upendeleo.
Naamini hayo yatatendewa kazi kwa udharula ili haki iweze kuonekana ikitendeka.
Peter Simon Msigwa: Mgombea-
M/kiti Kanda ya Nyasa.
Kufuatia madai haya Matukio Daima media tumemtafuta mgombea Uenyekiti Chadema Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi Sugu ili kuthibitisha tuhuma hizi ila Simu yake haikupokelewa japo jitihada za kumtafuta Bado zinaendelea .
0 Comments