Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa, amewakutanisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Ameyasema hayo leo Mei 28, 2024 wakati alipokuwa akifanya mahojiano na chombo cha habari ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.
Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga vizuri kuhakikisha inaboresha vivuko na kuweka machaguo kwa abiria ambapo watakuwa na chaguo.
"Ukitaka kutumia kivuko cha TEMESA sawa au ukitaka cha AZAM muda mchache kuvuka kwasababu zile ni ndogo siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja" Amesisitiza
Aidha amewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.
"Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunaofahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki" Amekaririwa Bashungwa
Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.
Bashungwa amesema Wizara inatambua changamoto ya wananchi ni huduma bora ya vivuko nakusema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu wataanza kutekeleza mpango huo utakaotoa wigo kwa wananchi kuchagua huduma wanayotaka kutumia.
"Wapo wanaotaka kushinikiza ili utaratibu na mwelekeo uende kama wanavyotaka wao, sisi hatuendi hivyo"amesema Bashungwa huku akisema kuwataja watu hao ni kuwapa sifa.
0 Comments