Header Ads Widget

WATENDAJI, VIONGOZI WA VIJIJI NA KATA ILEJE WAONYWA KUTOA VITAMBULISHO VYA NIDA KWA WAGENI

 .

Na Moses Ng'wat,Ileje.

SERIKALI imewataka Watendaj wa vijiji na kata Wilayani Ileje kuacha urasimu katika zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya urai (NIDA) kwa kuwa wananchi wanapaswa kupatiwa vitambulisho hivyo bila gharama yeyote, huku ikiwatahadhalisha kuepuka kutoa vitambulisho hivyo kwa  raia wa kigeni.


Tahadhali hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, leo Aprili 29, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Itale, Wilayani Ileje.


Chongolo amewataka watendaji hao na viongozi wa vijiji kuacha tabia ya kuwapa vibali wananchi kutoka nchi jirani kwa lengo la kupata vitambulisho vya uraia kwani inahatarisha usalama wa nchi pamoja na kudhulumu haki za watanzania, ikiwepo upatikanaji wa mbolea ya ruzuku.



"Acheni kuwaruhusu wananchi wasio raia wa Tanzania kupata vibali vya uraia kwani hali hiyo inawapa  upenyo raia hao wa kigeni kupata vitambulisho hivyo vya uraia na atakayebainika  atawajibika kwa mujibu wa sheria," amesema Chongolo.


Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji na viongozi hao  kujiepusha na urasimu wakati wa kugawa vitambulisho kwa wananchi kwa wananchi wanatakiwa kuvipata bila gharama yeyote.


Chongolo amesema Mkoa huo umepokea vitambilisho 35000 ambavyo vitagawiwa bure kwa wananchi waliojiandikisha hivyo kiongozi atakayebainika kuwatoza wananchi kwa gharama yoyote atashughulikiwa.


Hata hivyo, amewataka watumishi wa Nida kwenda vijijini kuwasajili wananchi ambao hawana vitambulisho kwani zoezi hili bado ni endelevu.


"Wananchi wote waliosajiliwa na ambao hawajasajiliwa wanahaki ya kupata vitambulisho ili kuwarahisishia kupata huduma za kijamii ambazo zinahitaji kuhudumiwa kwa kutumiwa vitambulisho hivyo," alisisitiza Chongolo.




Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS